Pages

Friday, January 17, 2014

MIGOGORO KUHUSU ARDHI ISIPUUZWE


                     Taarifa Maalumu kwa Vyombo vya Habari

                   MIGOGORO KUHUSU ARDHI ISIPUUZWE
                         Agricultural Council of Tanzania

Kila kukicha Tanzania inashuhudia kuibuka kwa migogoro na tafrani kuhusu ardhi katika sehemu nyingi nchini mwetu. Katika hali ya kawaida, Tanzania hapaswi kuwa na migogoro inayohusu ardhi kwa sababu tunayo tele ukiilinganisha na idadi ya wakazi wanaokadiriwa kuwa milioni 45 hivi.  Ukubwa wa ardhi yetu ni hekta milioni 94.5, kati ya hizo hekta milioni 44 ndizo zinazofaa kwa kilimo na ufugaji. Kati ya hekta hizi, ni takribani milioni 14 ndizo zinazotumiwa. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwepo kwa ardhi ya kutosha kwa wakulima na wafugaji.
Kama hali ndivyo ilivyo, kwa nini iwepo migogoro? Kwa maoni ya ACT, kuna sababu kadhaa, ambazo kwa hakika hazina mashiko. Sababu ambayo ni kubwa zaidi, ni Tanzania kutokuwa na ardhi ambayo ni rasmi kwa matumizi ya kilimo na ufugaji. Huwezi kuamini, lakini ukweli ni kwamba wakulima  na wafugaji wengi hawamiliki ardhi kisheria, ni sawa na wavamizi. Inakisiwa kwamba wanaomiliki ardhi kisheria, yaani wana hatimiliki, hawazidi asilimia mbili.  Cha ajabu ni kwamba Serikali yetu imetenga na kurasmisha ardhi kwa ajili: wanyamapori, misitu, uchimbaji wa madini, barabara, na maeneo ya miji.
Kwa kuwa wakulima na wafugaji hawakutengewa ardhi kwa matumizi yao, haishangazi kushuhudia hali ya kutoelewana mara kwa mara kati yao. Hasa inapodhihirika kwamba kuna tishio  la kuingiliana kimasilahi. Sasa mwingiliano huo umefikia hatua ya kuhatarisha maisha ya wananchi na mali zao. Hali hii ilianza kidogo kidogo na sasa imefikia pabaya sana. Hebu turejee mitafaruku ya hivi karibuni:
Mbarali
Kampuni ya Taifa ya Kilimo – NAFCO ilikuwa inamiliki Shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, lenye hekta 5,500 kwa ajili ya kilimo cha mpunga, na wanakijiji wapatao 4,400 wakimiliki hekta 1,870. Kwa msingi wa sera ya ubinafsishaji, Serikali ilimuuzia mwekezaji shamba hilo (Kapunga Rice Project), likijumuisha kwa makosa eneo la wanakijiji. Kwa hiyo anamiliki hekta 7,370. Sasa kumezuka mgogoro mkubwa kati ya mwekezaji na wanavijiji. Licha ya viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali kujaribu kutatua mgogoro huo, mpaka sasa bado hakuna muafaka. Serikali bado inajikanganya katika maamuzi.


Simanjiro
Wilayani Simanjiro kumeshamiri ugomvi wa kugombea ardhi kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji. Mara kwa mara  wazalishaji hao huzozana kuhusu umiliki na matumizi ya ardhi. Aidha, kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya wakazi wa kijiji cha Loiborsoi-A na mwekezaji mzalendo, Bw. Brown Ole Suya anayemiliki hekta 3,425. Malalamiko ya wananchi ni kwamba, ingawa mwekezaji huyo anayo hatimiliki ya mwaka 1992, hajaendeleza eneo lote. Kwa hiyo, anahodhi ardhi wakati wananchi majirani wanateseka kwa kukosa mahali pa kulima au kuchungia mifugo yao. ACT inashauri kwamba utaratibu wa kuhodhi ardhi, sharti ukomeshwe.
Kiteto 
Wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara hawana uhusiano mzuri kwa sababu ya kugombea ardhi mara kwa mara. Mapigano kati ya makundi hayo mawili yaliyoanza miaka minane iliyopita, yamesababisha majeruhi wengi, hata vifo. Hivi karibuni kulizuka mapigano makali katika Hifadhi ya Embroi Murtangosi. Mali nyingi ziliteketezwa kwa moto. Pia inakadiriwa watu wapatao kumi waliuwawa. Mtafaruku huo sasa umeshika kasi.
Kisarawe
Wananchi wengi wilayani Kisarawe wanalalamika kuhusu uporaji wa ardhi na wawekezaji kwa hila. Wawekezaji wengi wana tabia ya kukwepa utaratibu rasmi wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo. Badala ya kupitia vyombo vya Serikali, kwa mfano Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Mkoani na Wilayani, wao huenda moja kwa moja vijijini na kurubuni viongozi wa vijiji ili wapatiwe ardhi kwa utaratibu na masharti batilifu. Kwa kuwa karibu ardhi yote nzuri imeuzwa kwa kampuni za wageni, wanavijiji wanataabika kutokana na uhaba wa mashamba.
Mara nyingi uuzaji wa ardhi hugubikwa na ama usiri, au ghiliba - kwa maana ya wananchi kutofahamu athari zitokanazo. Mbaya zaidi, baadhi ya makampuni ya nje, badala ya kuzalisha mazao ya chakula, huamua kustawisha mazao yasiyo na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Kwa mfano, kustawisha mijatrofa, mitiiki/misaji, na pilipili hoho. Wilayani Kisarawe, kampuni iitwayo Sun Biofuel alimilikishwa hekta 8,210 kwa ajili ya kilimo cha jatrofa. 
Nini kifanyike 
Matatizo kama haya yanajirudiarudia nchi nzima. Mkuranga, Mvomero, Kilosa, Kilombero, Kiteto, Babati, Loliondo, Serengeti, Shinyanga, nakadhalika. Ni bomu linalosubiri kupasuka na kusababisha madhara makubwa ambayo yangeweza kuepukwa. Hivyo, kuna haja ya kuchukua tahadhari kabla bomu halijapasuka. Kwa hiyo, ACT inashauri ifuatavyo:
*  Ili kuondoa migongano katika matumizi ya ardhi, Serikali iandae Mpango wa Kitaifa wa 
    Matumizi ya Ardhi (National Land Use Plan). Aidha, iweke mipaka ambayo ni wazi na rasmi.  
    Mipaka hiyo iheshimiwe na wadau wote, vikiwemo vyombo vya Serikali. 

*  Wakulima na wafugaji waelimishwe kutambua ardhi iliyotengwa kwa matumizi yao. Vilevile, 
     watakaomilikishwa ardhi, wachukue jukumu la kuitunza na kuitumia vizuri, ikiwa ni pamoja 
     na kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti, na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

*  Sheria zinazohusu ardhi ambazo kwa sasa zinafanyiwa marekebisho, zitamke bayana kuwepo 
    kwa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kilimo na ufugaji. Aidha, ardhi hiyo itumiwe kwa ufanisi 
    kwa kuzingatia ikolojia, hali ya udongo, na mahitaji ya wakati huo.

*  Sheria na kanuni za ardhi zibainishe utaratibu wa kumiliki na kusimamia uendelezaji wa ardhi, 
     kwa kuzingatia madhumuni ya umilikishwaji wake. Kwa mfano: ardhi kwa ajili ya kilimo 
     isitumiwe vinginevyo bila sababu ya msingi. Endapo kuna mabadiliko ya lazima, vyombo 
     husika vijulishwe na viridhie.

*   Tabia ya kuhamahama ni miongoni mwa vyanzo vya kugombea ardhi. Iwekwe sheria ya 
     kudhibiti utamaduni huu. Wakulima na wafugaji wawe na makazi ya kudumu. Kuhamahama
     ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Mfano: mifugo kumomonyoa udongo, ukataji holela 
     wa miti, na uchomaji wa mkaa.

*   Utaratibu uliozoeleka ambao wawekezaji hupewa ardhi na vyombo vya juu kabisa bila 
     kushirikisha serikali za vijiji, mara nyingi hujenga uhasama usio wa lazima. Kwa hiyo, ni vema 
     kushirikisha ngazi za chini kuanzia wilaya, kata na vijiji husika. Kwani wenyeji wakielewa na 
     kuridhia, migogoro itapungua sana. 
     
*  Ardhi inayofaa kwa kilimo ipimwe, na wamiliki wapewe hatimiliki. Hii itakuwa na faida mbili. 
     Mosi, wakulima watakuwa na uhakika wa umiliki wa ardhi, hivyo kushawishika kuiendeleza 
     bila kusita. Pili, ardhi iliyopimwa na kupewa hatimiliki, ni dhamana tosha wakati wa kuomba 
     mikopo kutoka taasisi za kifedha.

*  Kuna haja ya kutoa huduma mahususi kwa wafugaji. Ardhi ya mifugo iwekewe miundombinu
     muhimu, kwa mfano mabwawa ya kunyweshea wanyama, majosho, na njia maalumu za 
     kufikia sehemu hizo. Aidha, wafugaji waelimishwe umuhimu wa kustawisha nyasi (malisho)
     kwa ajili ya mifugo yao. 

*  Endapo kuna haja ya kuchukua ardhi ya wakulima au wafugaji kwa manufaa ya umma, sharti 
    la kwanza waathirika waelimishwe kuhusu kusudio hili. Mchakato mzima uwe wazi. Aidha, 
    waanga wa zoezi hilo, sharti walipwe fidia stahiki.

*  La muhimu zaidi, ACT inasihi viongozi (hasa watendaji wakuu) wa vyombo vya Serikali 
    vinavyohusika, wajenge utamaduni wa kufika haraka katika maeneo ambayo yanaonyesha
    dalili za kulipuka kwa mzozo. Jukumu lao la kwanza ni kutuliza hali hiyo, pamoja na 
    kufanikisha suluhisho la kudumu. Ingawa sio rahisi kuridhisha kila mtu, lakini viongozi hao 
    wajitahidi kutenda haki kwa wahusika, bila kuegemea upande wowote.

TFF YANOA MAKATIBU MABORESHO TAIFA STARS


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya siku mbili kwa makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuhusu maboresho ya timu ya Taifa (Taifa Stars).

Semina hiyo inafanyika ukumbi wa Singida Motel, mjini Singida kuanzia kesho (Januari 18 mwaka huu) ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa kwa washiriki kuhusu maboresho hayo.

TFF imeandaa mpango wa maboresho kwa Taifa Stars ambapo pamoja na mambo mengine umepanga kusaka vipaji nchini nzima kwa lengo la kupanua wigo wa kupata wachezaji wanaoweza kuchezea timu hiyo.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager mwaka huu inakabiliwa na mechi za mchujo za Kombe la Afrika (AFCON) ambalo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Morocco.

Mechi hizo za mchujo zitachezwa kati ya Septemba na Novemba mwaka huu ili kupata timu 16 zitakazofuzu kucheza fainali hizo.

WASOMALI KUCHEZESHA YANGA, WACOMORO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Somalia kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Komorozine Sports ya Comoro.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mchujo itafanyika jijini Dar es Salaam kati ya Februari 7 na 9 mwaka huu wakati ile ya marudiano itachezwa kisiwani Comoro kati ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Mwamuzi wa kati atakuwa Hassan Mohamed Hagi wakati wasaidizi wake ni Hamza Hagi Abdi, Bashir Abdi Suleiman na Bashir Olab Arab. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Eugene Musoke kutoka Uganda.

Timu ambazo zimeingia moja kwa moja katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ni Coton Sport ya Cameroon, El Ahly (Misri), TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Hilal (Sudan), Club Sportif Sfaxien (Tunisia) na Esperance (Tunisia) 

Nayo mechi ya kwanza ya raundi ya mchujo kati ya Azam ya Tanzania na Ferroviario Da Beira ya Msumbiji itakayofanyika Dar es Salaam kati ya Februari 7 na 9 mwaka huu itachezeshwa na waamuzi kutoka Sudan.

Waamuzi hao ni Mutaz Abdelbasit Khairalla atakayepuliza filimbi, Waleed Ahmed Ali, Aarif Hasab Elton na El Fatih Wadeed Khaleel. Kamishna wa mechi hiyo ni Hassan Mohamed Mohamed kutoka Somalia. Mechi ya marudiano itachezwa Msumbiji kati ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Timu zilizotinga moja kwa moja katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Ismailia (Misri), Wadi Degla (Misri), Djoliba (Mali), MAS (Morocco), Bayelsa United (Nigeria), El Ahly Shandy (Sudan), E.S.S. (Tunisia), C.A.B. (Tunisia) na Zesco United (Zambia).

WATANZANIA KUCHEZESHA MECHI ZA CL, CC
Watanzania wanane wameteuliwa kuchezesha mechi mbili za marudiano za raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) na Kombe la Shirikisho (CC) zitakazochezwa wikiendi ya Februari 14 na 16 mwaka huu.

Waamuzi hao walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Israel Mujuni atakayechezesha mechi ya CL kati ya Rayon Sport ya Rwanda na AC Leopards de Dolisie ya Congo itakayofanyika jijini Kigali.

Mujuni atasaidiwa na Josephat Bulali, Samwel Mpenzu na Ramadhan Ibada, wakati Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Jean Marie Hicuburundi wa Burundi.

Naye Waziri Sheha ataongoza jopo lingine kwenye mechi ya CC kati ya FC MK ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na El Ahly Atbara ya Sudan. Mechi hiyo itachezwa jijini Kinshasa.

Sheha atasaidiwa na Ferdinand Chacha, John Kanyenye na Israel Mujuni. Kamishna wa mechi hiyo ni Chayu Kabalamula kutoka Zambia.

SEMINA YA KUPANDISHA MADARAJA WAAMUZI JAN 21
Semina kwa ajili ya kupandisha madaraja waamuzi itafanyika Januari 21 na 22 mwaka huu katika vituo vitatu vya Dodoma, Mwanza na Songea.

Waamuzi watakaoshiriki katika semina hizo ambazo pia zitahusisha mitihani ya utimamu wa mwili (physical fitness test) watajigharamia wenyewe na wanatakiwa kufika vituoni siku moja kabla. Waamuzi hao ni wa daraja la pili na tatu.

Kituo cha Dodoma kitahusisha waamuzi kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Pwani, Singida na Tanga. Wakufunzi katika kituo hicho ni Paschal Chiganga, Said Nassoro na Soud Abdi.

Wakufunzi wa kituo cha Mwanza kwa ajili ya waamuzi wa mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora ni Alfred Kishongole, Kanali Issarow Chacha, Saloum Chama na Zahra Mohamed.

Kituo cha Songea ni kwa ajili ya waamuzi kutoka Iringa, Lindi, Mbeya, Mtwara, Njombe, Rukwa na Ruvuma. Wakufunzi katika kituo hicho ni Charles Ndagala, Joseph Mapunda, Riziki Majala na Victor Mwandike.

Waamuzi wote wanatakiwa kwenda katika kituo walichapangiwa. Vilevile wanatakiwa kuwa na barua kutoka kwa makatibu wa Vyama vya Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) wa mikoa yao ikiwatambulisha pamoja na kuonesha madaraja yao.   


MKUU WA MKOA WA RUKWA AONANA NA TIMU MAALUM YA KUHAKIKI MAENEO MAPYA YA UTAWALA KUTOKA TAMISEMI, AISHAURI MAMLAKA HUSIKA KUANGALIA UPYA VIGEZO VINAVYOTUMIKA KUGAWA MAENEO MAPYA YA UTAWALA



Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akizungumza na timu maalum inayohakiki maeneo mapya ya utawala kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Pichani kulia na timu yake ya Mkoa iliyokuwa ikiratibu maeneo hayo ofisini kwake leo tarehe 17 Januari 2014. Timu hiyo kutoka TAMISEMI inaongozwa na Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard Ngatale (watatu kulia).

Katika kikao hicho kifupi Mkuu huyo wa Mkoa ameiomba mamlaka husika kupitia timu hiyo kuangalia upya vigezo vinavyotumika katika kugawa maeneo mapya ya utawala na upandishaji wa madaraja kutoka kijiji, kata, Tarafa, Halmashauri, Miji na Manispaa. 

Alisema kuwa kuna maeneo mengine ambayo yakiangaliwa kwa kigezo kimoja cha wingi wa watu bila kuangalia umbali wa huduma na giografia ya eneo husika unakuta wananchi wanakosa huduma zao za msingi na kupata tabu kubwa katika kuzipata.

 Alitolea mfano vijiji vikubwa vya mwambao ambavyo kupata huduma katika kata zao ni lazma wavuke upande mmoja wa Ziwa kwenda upande mwingine jambo ambalo ni hatarishi kama ilivyotokea kwa wananchi wa Kijiji cha Kipwa Mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambao hivi karibuni walipoteza watu 15 katika ajali ya boti walipokwenda kupata huduma ya afya. Wengi ya waliofariki katika ajali hiyo mbaya walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka 5.  
 Kikao kikiwa kinaendelea ambapo kwa upande wake Mwanasheria wa TAMISEMI Ndugu Eustard Ngatale alisema kuwa kubariki na kuhalalisha uanzishwaji wa maeneo mapya ya Utawala vipo vitu mbalimbali vya kuzingatia ambavyo ni pamoja na kuwepo kwa makubaliano ya wananchi na viongozi wa maeneo husika kupitia mihutasari ya vikao maalumu vya kisheria vya WDC, Halmashauri, DCC na RCC katika ngazi ya Mkoa.
(Na Hamza Temba – Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)


SERIKALI YA TANZANIA KUENDELEA KUIMARISHA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam juu ya  Shirikika la ndege la Tanzania (ATCL) kupanua huduma zake na kufika Bujumbura nchini Burundi, ATCL ilianza kufanya safari zake kati ya Tanzania na Burundi Desemba16, 2013 mara tatu kwa wiki kama moja ya hatua za kuimarisha usafiri wa anga kati ya nchi wanachama. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo

Na Frank Mvungi

Serikali ya Tanzania imedhamiria kuimarisha ushirikiano baina yake na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Nyanja za miundombinu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Samuel Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

Mh.Sitta alibainisha kuwa mwishoni mwa mwaka 2013 Mawaziri wa Tanzania, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walikutana kujadili namna ya kuimarisha miundo mbinu ya barabara, reli, anga, anga na maji.

Mh.Sitta aliongeza kuwa katika kikao hicho ilikubaliwa kuwa Shirikika la ndege la Tanzania (ATCL) lipanue huduma zake na kufika Bujumbura nchini Burundi ambapo ATCL ilianza kufanya safari zake kati ya Tanzania na Burundi Desemba16, 2013 mara tatu kwa wiki kama hatua za awali za utekelezaji.

Mh. Sitta alisisitiza kuwa katika mkutano wa 8 wa Baraza la la Mawaziri la Jumuiya hiyo umeridhia mfumo wa himaya moja ya Forodha na mpangokazi unaoainisha masuala ya utekelezaji katika kipindi cha miezi sita ili kuwezesha kuanzishwa kwa himaya hiyo ifikapo Juni 2014.

Mh. Sitta akifafanua zaidi alisema mfumo wa himaya moja ya forodha unaainisha utaratibu wa mzunguko wa biashara, usimamizi wa mapato na mfumo wa kisheria.

Katika mfumo huo Sitta alisema kuwa ilikubalika kuwa nchi wanachama zitakusanya mapato yake ya kodi.

Aidha, kwa bidhaa zinazopitia nchi moja kuelekea nchi nyingine wanachama za Jumuiya hiyo zimekubaliana kuwa nchi husika itakusanya mapato yake na kuifahamisha mamlaka ya forodha mizigo ilipoingilia katika Jumuiya kwa kwa ajili ya kuruhusu bidhaa kuondoshwa.

Mkutano wa 15 wa Kawida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki Uliofanyika Jijini Kampala, Uganda Novemba 30, 2013 na kuamua masula muhimu ya maendeleo ya Mkutano wa Jumuiya Afrika Mashariki.

Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kutolewa uamuzi ni pamoja na kutiwa saini kwa Itifaki ya Umoja wa Fedha, kuidhinishwa uundwaji wa Himaya ya Umoja wa Forodha (Single Customs Territory).



SHIRIKA LA NYUMBA LATOA MAFUNZO KWA VIKUNDI VYA VIJANA,LENGO NI KUBADILI MAISHA YAO



Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba nchini (NHC), Bw. Nehemia Kyando Mchechu akizungumza wakati wa maadalizi ya ufungaji wa mafunzo ya vijana wawakilishi wa vikundi kutoka mikoa mbalimbali kuhusu utengenezaji wa matofali ya udongo yenye teknolojia ya Interlocking Blocks yaliyoanza Januari 6 mpaka 17 mwaka huu ambayo yanatarajiwa kufungwa wiki ijayo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda, Mkurugenzi huyo amesema Shirika la nyumba badala ya kwenda kutoa msaada wa sabuni na vyakula katika vituo vya watoto yatima au kusaidia biskuti limeamua kubadilisha maisha ya vijana wa Tanzania kwa kuwapa mafunzo na kuwapatia mashine za kutengeneza matofali ya udongo ambayo wao NHC watakuwa ndiyo wateja wakuu wa kununa matofali hayo, lakini pia shirika hilo linatoa mashine za kufyatulia matofali zipatazo 640 katika wilaya 160 mikoa yote ya Tanzania bara na kiasi cha shilingi 500,000 kila mkoa kama mtaji wa kununulia saruji kwa vikundi hivyo, Katikati ni Injinia Kwanama Elias Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo kutoka Nation Housing&Building Research Agency (NHBRA) na kushoto ni Bw.Julius Njelwa kutoka VETA, mafunzo hayo yameratibiwa kwa pamoja na (NHC), (VETA) na (NHBRA) kwa pamoja.

 Injinia Kwanama Elias Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo kutoka Nation Housing&Building Research Agency (NHBRA) akifafanua masuala ya kitaalamu kuhusu teknolojia hiyo ya matofali kwa waandishi wa habari.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo. Baadhi ya maofisa wa Shirika la Nyumba NHC wakiwa katika maadalizi hayo kushoto ni Suzan Omary Meneja Mawasiliano NHC, Muungano Saguya Meneja huduma kwa jamii NHC na Ephraim Kibonde mtangazaji wa Clouds Radio.



WAZIRI MKUU AKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO MPWAPWA


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama sehemu ya jengo la Kituo cha Polisi cha kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa ambayo imeporomoka kufuatia mafuriko yaliyokikumba kijiji hicho kufuatia mvua kubwa zianazoendelea kunyesha mkoani Dodoma januari 17, 2014. Kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dr. Rehema Nchimbi.

 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua athari za mafuriko yaliyokikumba kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa Januari 17, 2014. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Mpwapwa, Gregory Tewu na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dr. Rehema Nchimbi.
 Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akikagua daraja ambalo lilizibwa na maporomoko ya maji yaliyoambatana na magogo , mawe na udongo na kusababisha mafuriko katika kijiji cha Chipogoro wilayani Mpwapwa januari 17,20134.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikagua athari za mafuriko katika kijiji cha Fufu wilayani Chamwino, Dodoma, Januari 17, 2014.Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rehema nchimbi na kulia kwake ni Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Tuesday, January 14, 2014

WACHEZAJI 30 TWIGA STARS WAITWA KUIVAA ZAMBIA


30 TWIGA STARS WAITWA KUIVAA ZAMBIA
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ametaja kikosi cha wachezaji 30 wanaoingia kambini kesho (Januari 15 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi dhidi ya Zambia mwezi ujao.

Mechi hiyo ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika baadaye mwaka huu jijini Windhoek, Namibia itafanyika jijini Lusaka.

Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni Amina Ally (Lord Baden Sekondari), Amisa Athuman (Marsh Academy), Anastazia Anthony (Lord Baden Sekondari), Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar) na Belina Julius (Lord Baden Sekondari).

Donisia Daniel (Lord Baden Sekondari), Esther Chabruma (Sayari Queens), Evelyn Sekikubo (Kwimba Chuoni), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Hassan (Mburahati Queens), Fatuma Issa (Evergreen) na Fatuma Mustapha (Sayari Queens).

Fatuma Omari (Sayari Queens), Happiness Hezron (Copa Coca-Cola Ilala), Maimuna Hamisi (U20 Tanzanite), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Real Tanzanite), Mwapewa Mtumwa (Sayari Queens), Najiat Abbas (Makongo Sekondari) na Neema Paul (U20 Tanzanite).

Pulkeria Charaji (Sayari Queens), Semeni Abeid (Real Tanzanite), Shelder Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Sayari Queens), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).

RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MMARI
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mwanzilishi wa wa timu ya Oljoro JKT, Kanali Mmari kilichotokea jana (Januari 13 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Kanali Mmari ambaye aliasisi timu hiyo na kuifikisha hadi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom amefia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa baada ya kupata ajali ya gari Chalinze mkoani Pwani, Januari Mosi mwaka huu.

Msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira wa miguu kwani mbali kuasisi timu ya Oljoro JKT alikuwa mhamasishaji mkubwa wa mchezo huo mkoani Arusha, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mmari, klabu ya Oljoro JKT, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

MAOFISA TFF KUKAGUA VIWANJA 19 VYA VPL, FDL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeteua maofisa wanaoanza leo (Januari 14 mwaka huu) kukagua viwanja 19 vitakavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Ukaguzi huo pia unahusisha viwanja ambavyo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilizuia mechi za VPL na FDL kuchezwa mpaka hapo vitakapokuwa vimefanyiwa marekebisho ili kukidhi sifa za kutumiwa kwa mechi hizo.

Viwanja vinavyokaguliwa ni Ali Hassan Mwinyi (Tabora), CCM Kirumba (Mwanza), Jamhuri (Dodoma), Jamhuri (Morogoro), Kaitaba (Bukoba), Kambarage (Shinyanga), Kumbukumbu ya Karume (Musoma) na Kumbukumbu ya Samora (Iringa).

Kumbukumbu ya Sokoine (Mbeya), Lake Tanganyika (Kigoma), Mabatini (Pwani), Majimaji (Songea), Mbinga (Mbinga), Mkwakwani (Tanga), Mwadui (Shinyanga), Wambi (Mufindi, Iringa), Sheikh Kaluta Amri Abeid (Arusha), Umoja (Mtwara) na Vwawa (Mbozi).

Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika na mameneja wa viwanja husika wanatakiwa kuwapa ushirikiano wakaguzi hao kutoka TFF.

RAIS MALINZI KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI LEO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa semina ya waamuzi na makamisha leo (Januari 14 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa mikutano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50 wameshiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) wakati waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.
 
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

NASRI WA MAN CITY AJERUHIWA VIBAYA


Mchezaji wa kiungo cha kati, wa Manchester City Samir Nasri, atafanyiwa uchunguzi zaidi wa jereha la goti alilopata wakati wa mechi ya klabu hiyo dhidi ya Newcastle.

Nasri aliondoshwa uwanjani baada ya kufanyiwa masihara na Mapou Yanga wakati wa mechi yao ambapo walishinda mabao mawili kwa nunge.

Kocha wa City Manuel Pellegrini alighadhabishwa mno na tukio hilo na kusema kuwa mtu aliyepaswa kuadhibiwa ni Yanga-Mbiwa.

"Nasri amepata jeraha baya sana. Ilipaswa kuwa kadi nyekundu kwa Yanga,'' alisema Pellegrini.

"alijeruhiwa vibaya lakini tutajua hali yake Jumatatu,'' aliongeza kusema kocha huyo.

Meneja wa Newcastle hata hivyo alimtetea Yanga-Mbiwa.

"Haikuwa nia yake kumjeruhi Nasri," alisema kocha Pardew. " hiyo sio kawaida yake na natumai kuwa Nasri yuko salama.''

Nasri ambaye huchezea timu ya kitaifa ya Ufaransa, aliondoka uwanjani dakika ya 79 na kupokea matibabu kwa dakika chache, kabla ya kuondoka akiwa analia kwa uchungu.

Yanga-Mbiwa hata hivyo alipata onyo la refa.

Kocha Pellegrini pia alithibitisha kuwa Edin Dzeko, aliyeingiza bao lililowapa ushindi City na kuwaweka katika nafasi ya kwanza katika ligi ya premier, alipata jeraha la mguu.
SOURCE:  BBC

RONALDO NDIYE MCHEZAJI BORA WA DUNIA KWA MWAKA 2013


Mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo jana usiku alinyakua tuzo ya mchezajii bora wa soka wa FIFA wa mwaka 2013 na kuwashinda Lionel Messi wa Barcelona na Frank Ribery wa Bayern Munich.

Ronaldo ambaye alinyakuwa tuzo hiyo ya mchezaji bora wa dunia kwa mara kwanza mwaka 2008 alitangazwa kunyakua tuzo mwaka 2013 baada ya kupigiwa kura na makocha, manahodha na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa matokeo Ronaldo alipata kura 1365 akimshinda Messi aliyepata kura 1,205 na Ribery akiambulia kura 1,127.

Kwa upande wa wanawake golikipa wa Ujerumani Nadine Angerer alinyakuwa tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa soka kwa upande wa wanawake huku aliyekuwa kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes akinyakua tuzo ya kuwa kocha bora wa dunia.
SOURCE:  BBC

HALI YA HEWA: UPEPO MKALI WAJA PWANI

Kutokana na hali hiyo tunawatahadharisha watumiaji wa bahari na wakazi wa maeneo hatarishi kuchukua tahadhari,”  imesema sehemu ya taarifa hiyo. (PICHA MAKTABA )
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kutokea kwa upepo mkali katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi Mtwara na Visiwa vya Unguja na Pemba na imewataka wananchi kuwa waangalifu.

Aidha mamlaka hiyo imesema kuwa sambamba na upepo huo mkali, pia kunatazamia kutokea mvua kali kwenye mikoa ya Rukwa, Mbeya ,Njombe, Mtwara, Ruvuma na Morogoro.

Taarifa ya mamlaka hiyo ilisema kwamba hali hiyo inatokana na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi na maeneo ya Mkondo wa Msumbiji.

Imesema kuwa mfumo huu unatarajiwa kuvuta upepo kutoka Pwani ya Somalia na misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

“Mamlaka inatahadharisha kuwa kuanzia leo hadi Januari 16, kunatarajiwa kujitokeza upepo mkali unaozidi kilometa 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa zaidi ya 2.0.

Kutokana na hali hiyo tunawatahadharisha watumiaji wa bahari na wakazi wa maeneo hatarishi kuchukua tahadhari,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mamlaka hiyo imesema kuwa kiwango cha mvua kinatarajiwa kuongezeka hadi kufikia kiwango cha milimita 50 kwa saa 24 ikiwa ni wastani wa asilimia 60.

“Hata hivyo mamlaka inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo pale inapobidi, lakini tunasisitiza kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari,” imesema taarifa hiyo.

Tahadhari hii imekuja wakati Watanzania bado wanakumbuka nyingine iliyotolewa ndani ya wiki mbili zilizopita na siku chache baadaye vyombo viwili vya abiria vilivyokuwa vikisafiri Bahari ya Hindi kupata ajali na kusababisha vifo vya watu tisa.

Ajali zote mbili zilitokea Januari 5 mwaka huu, moja ikitokea karibu na eneo la Visiwa vya Mafia na nyingine eneo la Nungwi lililopo kati ya Unguja na Pemba.

Ajali iliyotokea Nungwi iliihusisha boti ya Kilimanjaro II baada ya kukumbwa na dhoruba.

KIBONZO CHA LEO..............!!

JAJI LIUNDI, HASHIM SAGGAF WAFARIKI DUNIA

Waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa Jaji, George Liundi nyumbani kwake, Keko jijini Dar es Salaam jana.  Jaji huyo anatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi ya Chang'ombe keshokutwa.
Taifa limepoteza watu wawili mashuhuri. Hao ni Msajili wa Kwanza wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji George Liundi (78) na Mbunge wa zamani wa Dodoma Mjini, Hashim Saggaf.

Jaji Liundi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana alipokuwa akipelekwa Hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu wakati Saggaf, ambaye alikuwa Diwani wa Mtafukoge, Dar es Salaam alifariki jana saa nne asubuhi kwenye Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Saggaf alizikwa jana kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam na mazishi ya Jaji Liundi yamepangwa kufanyika keshokutwa.

Jaji Liundi
Jaji Liundi alikuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, mwaka mmoja baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, Julai mosi, 1993 na alistaafu mwaka 2001 na nafasi yake kuchukuliwa na John Tendwa ambaye naye alistaafu Agosti, mwaka jana na kumuachia kijiti, Jaji Francis Mutungi.

Wakati akiianza kazi hiyo, mfumo wa vyama vingi ulikuwa hauna nguvu, huku vyama vya siasa vikiwa vichache na kikubwa cha upinzani kilikuwa NCCR-Mageuzi.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, Keko Juu, Dar es Salaam, msemaji wa familia ambaye pia ni mtoto wa kwanza wa marehemu Liundi, Taji alisema baba yake kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo.

Alisema alikuwa yu mtu mwenye afya njema, lakini siku tatu zilizopita alikuwa akilalamika zaidi kuumwa mgongo.

“Afya yake ilikuwa nzuri licha ya kuwa alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu (BP), alikuwa akipatiwa matibabu kila alipokuwa akijisikia vibaya, kifupi alikuwa katika hali nzuri,” alisema Taji na kuongeza:

“Ijumaa na Jumamosi iliyopita nilimpeleka kwa daktari wake na kupatiwa matibabu. Jumapili (juzi) aliamka akiwa na afya nzuri,” alisema Taji.

Alisema hali ya Liundi ilibadilika ghafla usiku wa kuamkia jana, huku akiwa analalamika kuumwa mgongo... “Niliamua kumpeleka TMJ lakini tukiwa njiani, alifariki dunia.”

Taji alisema sasa wanasubiri ripoti ya madaktari, lakini wanaamini ugonjwa uliyomuua baba yao ni malaria kali. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
 
Alisema misa ya kumuombea Jaji Liundi itafanyika kwenye Kanisa Katoliki Chang’ombe wilayani Temeke, Alhamisi na mazishi yatafanyika katika Makaburi ya Chang’ombe.

Marehemu Liundi ameacha watoto watatu na mjane mmoja.

Jaji Liundi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1980.

Pia amefanya kazi katika nchi mbalimbali zikiwamo Zambia, Zimbabwe na Uswisi

Alikuwa mmoja wa Watanzania waliotengeneza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.”

Wanasiasa wamlilia

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alieleza kustushwa na taarifa za msiba huo na kusema anakumbuka ushirikiano wake kwa vyama vya siasa.

“Nawapa pole ndugu zake, watoto na mkewe kwa kumpoteza mtu muhimu, hiyo ndiyo njia tutakayopitia wote. Liundi alikuwa mtu mwadilifu nasikitika sana kusikia kifo chake,” alisema Mtei.

Kwa upande wake, Tendwa alisema Liundi anapaswa kuenziwa na Watanzania wote kwa kuasisi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi... “Watanzania wanatakiwa kumpa heshima kwa sababu yeye ndiye aliyeasisi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na michakato yote, zikiwamo sheria mbalimbali zilizopo hadi sasa.

“Yeye ndiye aliyesajili vyama vya awali vya upinzani mbali na CCM vikiwamo CUF, Chadema, TPP ambacho baadaye kilifutwa na vingine vingi. Alisimamia chaguzi za awali tangu mwaka 1994 hadi 1995. Alijitahidi kuubeba mfumo huo ukiwa bado mchanga… kimsingi yeye ndiye aliyetuwekea dira na kujenga msingi tulioukuta sisi, bila yeye tusingefika hapa tulipo.”

Nyuki wavuruga mazishi ya Saggaf
Waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya Saggaf walilazimika kukimbia kusaka hifadhi ya muda baada ya kundi kubwa la nyuki kuvamia eneo la makaburi saa kumi jioni.

Mtu mmoja, ambaye inaelezwa alikuwa na tatizo la kutoona vizuri alishambuliwa vikali na wadudu hao na kupelekwa Hospitali ya Regency kwa matibabu.

Hali ilitulia baada ya saa moja hivi na kutoa fursa ya shughuli za maziko kuendelea.

Mtoto wa marehemu, Ahmed Saggaf alisema baba yake alifariki baada ya kulazwa kwa siku tano kutokana na matatizo ya figo na ini.

Ahmed alisema kisomo cha kumuombea marehemu kitafanyika leo katika Msikiti wa Kipwata, Kariakoo, Dar es Salaam.

Saggaf alikuwa Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

WATU 10 WAUAWA KITETO, MTWARA JAMBAZI LAUA POLISI

Dodoma na Mtwara. 
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika Hifadhi ya Embroi Murtangosi, wilayani Kiteto mkoani Manyara, imefikia 10.

Wakati hayo yakiendelea, huko Mtwara askari polisi wawili na raia mmoja wameuawa kwa kupigwa risasi na jambazi. Kuongezeka kwa idadi ya waliokufa huko Kiteto, kunafuatia kupatikana kwa miili ya watu wengine watatu katika Kitongoji cha Mtanzania. Awali ilielezwa kuwa watu sita walikuwa wameuawa katika mapigano hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla, alisema watu hao watatu wamefariki dunia jana baada ya kushambuliwa na wafugaji wa jamii ya Kimasai.

Alisema “hali ya usalama katika hifadhi hiyo, bado haijatengemaa na kwamba watu wanaendelea kukimbia.”

Mkuu huyo wa wilaya alisema alifika katika kitongoji hicho na kushuhudia miili ya watu hao ambao kwa sasa wamehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ikisubiri kutambuliwa. Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima na Wafugaji wilayani humo (Chawaki), Hassan Losiyoki, alisema hali si shwari na kwamba watu bado wanauawa.

Mapigano hayo yamedumu kwa miaka minane na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 20 na wengine 14 kujeruhiwa.

Kutoka Mtwara. Abdallah Nasoro anaaripoti kuwa watu watatu wakiwamo askari polisi wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi katika Wilaya ya Newala. mwingine, amevunjwa kiuno.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, zilisema tukio hilo lilitokea juzi jioni katika Msitu wa Kijiji cha Kiduni, ambako majambazi yalikimbilia baada ya kupora fedha kutoka kwenye kituo cha mafuta kilichopo katika kijiji hicho. Habari hizo zilisema katika tukio hilo, majambazi walimuua mwananchi mmoja kwa kumpiga risasi kisha kupora fedha ambazo hazijafahamika ni kiasi gani na kutokomea msituni.

Kwa mujibu wa habari hizo, polisi waliwafuta majambazi hayo na kuanza kujibizana kwa risasi.

Inasemekana wakati wakiendelea na mapambano jambazi mmoja alitokomea na kumwacha mmoja ambaye alikuwa na silaha mkononi akiendelea na mapambano.

Baadaye jambazi huyo alinyoosha mikono juu kama ishara ya kujisalimisha na ndipo askari wawili walipomfuata kwa lengo la kumkamata, lakini ghafla alichukua silaha yake na kuwafyatulia risasi na kufa papo hapo.

Imeelezwa kuwa katika harakati za kuokoa maisha yake askari mmoja ambaye alikuwa dereva wa gari la polisi, alipigwa risasi ya kiuononi na kusababisha kuvunjika kwa sehemu hiyo ya mwili.

Habari zinasema polisi wanaendelea na msako dhidi ya majambazi hao.

WAISLAMU KUSHEREHEKEA MAULIDI LEO

Muumini wa Dini ya Kiislam Mohamad Abdulkadir, akipamba taa kwenye msikiti wa Faizan-E-Madina kwa ajili ya mkesha wa Sikukuu ya Maulid inayofanyika leo.
Waumini mbalimbali wa dini ya Kiislamu nchini, wanaungana na wenzao duniani kote leo katika mapumziko ya kuadhimisha Sikukuu ya Maulid ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) miaka 1345 iliyopita.

Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shaaban Simba alisema jana kuwa, kitaifa Maulid hayo yalifanyika jana usiku mkoani Kigoma.

Alisema Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba ndiye aliyeongoza Maulid hayo kitaifa na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa huo, Issa Machibya.

Simba alitumia fursa hiyo kuwatakiwa Watanzania wote mapumziko mema ya Maulid kwa kusherehekea kwa amani na kuepuka kujihusisha na vitendo viovu.

“Tunawaomba wananchi kutumia mapumziko haya vizuri kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema Simba. Jijini Dar es Salaam, maadhimisho hayo yalifanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.