Pages

Friday, January 17, 2014

MIGOGORO KUHUSU ARDHI ISIPUUZWE


                     Taarifa Maalumu kwa Vyombo vya Habari

                   MIGOGORO KUHUSU ARDHI ISIPUUZWE
                         Agricultural Council of Tanzania

Kila kukicha Tanzania inashuhudia kuibuka kwa migogoro na tafrani kuhusu ardhi katika sehemu nyingi nchini mwetu. Katika hali ya kawaida, Tanzania hapaswi kuwa na migogoro inayohusu ardhi kwa sababu tunayo tele ukiilinganisha na idadi ya wakazi wanaokadiriwa kuwa milioni 45 hivi.  Ukubwa wa ardhi yetu ni hekta milioni 94.5, kati ya hizo hekta milioni 44 ndizo zinazofaa kwa kilimo na ufugaji. Kati ya hekta hizi, ni takribani milioni 14 ndizo zinazotumiwa. Takwimu hizi zinadhihirisha kuwepo kwa ardhi ya kutosha kwa wakulima na wafugaji.
Kama hali ndivyo ilivyo, kwa nini iwepo migogoro? Kwa maoni ya ACT, kuna sababu kadhaa, ambazo kwa hakika hazina mashiko. Sababu ambayo ni kubwa zaidi, ni Tanzania kutokuwa na ardhi ambayo ni rasmi kwa matumizi ya kilimo na ufugaji. Huwezi kuamini, lakini ukweli ni kwamba wakulima  na wafugaji wengi hawamiliki ardhi kisheria, ni sawa na wavamizi. Inakisiwa kwamba wanaomiliki ardhi kisheria, yaani wana hatimiliki, hawazidi asilimia mbili.  Cha ajabu ni kwamba Serikali yetu imetenga na kurasmisha ardhi kwa ajili: wanyamapori, misitu, uchimbaji wa madini, barabara, na maeneo ya miji.
Kwa kuwa wakulima na wafugaji hawakutengewa ardhi kwa matumizi yao, haishangazi kushuhudia hali ya kutoelewana mara kwa mara kati yao. Hasa inapodhihirika kwamba kuna tishio  la kuingiliana kimasilahi. Sasa mwingiliano huo umefikia hatua ya kuhatarisha maisha ya wananchi na mali zao. Hali hii ilianza kidogo kidogo na sasa imefikia pabaya sana. Hebu turejee mitafaruku ya hivi karibuni:
Mbarali
Kampuni ya Taifa ya Kilimo – NAFCO ilikuwa inamiliki Shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, lenye hekta 5,500 kwa ajili ya kilimo cha mpunga, na wanakijiji wapatao 4,400 wakimiliki hekta 1,870. Kwa msingi wa sera ya ubinafsishaji, Serikali ilimuuzia mwekezaji shamba hilo (Kapunga Rice Project), likijumuisha kwa makosa eneo la wanakijiji. Kwa hiyo anamiliki hekta 7,370. Sasa kumezuka mgogoro mkubwa kati ya mwekezaji na wanavijiji. Licha ya viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali kujaribu kutatua mgogoro huo, mpaka sasa bado hakuna muafaka. Serikali bado inajikanganya katika maamuzi.


Simanjiro
Wilayani Simanjiro kumeshamiri ugomvi wa kugombea ardhi kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji. Mara kwa mara  wazalishaji hao huzozana kuhusu umiliki na matumizi ya ardhi. Aidha, kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya wakazi wa kijiji cha Loiborsoi-A na mwekezaji mzalendo, Bw. Brown Ole Suya anayemiliki hekta 3,425. Malalamiko ya wananchi ni kwamba, ingawa mwekezaji huyo anayo hatimiliki ya mwaka 1992, hajaendeleza eneo lote. Kwa hiyo, anahodhi ardhi wakati wananchi majirani wanateseka kwa kukosa mahali pa kulima au kuchungia mifugo yao. ACT inashauri kwamba utaratibu wa kuhodhi ardhi, sharti ukomeshwe.
Kiteto 
Wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara hawana uhusiano mzuri kwa sababu ya kugombea ardhi mara kwa mara. Mapigano kati ya makundi hayo mawili yaliyoanza miaka minane iliyopita, yamesababisha majeruhi wengi, hata vifo. Hivi karibuni kulizuka mapigano makali katika Hifadhi ya Embroi Murtangosi. Mali nyingi ziliteketezwa kwa moto. Pia inakadiriwa watu wapatao kumi waliuwawa. Mtafaruku huo sasa umeshika kasi.
Kisarawe
Wananchi wengi wilayani Kisarawe wanalalamika kuhusu uporaji wa ardhi na wawekezaji kwa hila. Wawekezaji wengi wana tabia ya kukwepa utaratibu rasmi wa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo. Badala ya kupitia vyombo vya Serikali, kwa mfano Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Mkoani na Wilayani, wao huenda moja kwa moja vijijini na kurubuni viongozi wa vijiji ili wapatiwe ardhi kwa utaratibu na masharti batilifu. Kwa kuwa karibu ardhi yote nzuri imeuzwa kwa kampuni za wageni, wanavijiji wanataabika kutokana na uhaba wa mashamba.
Mara nyingi uuzaji wa ardhi hugubikwa na ama usiri, au ghiliba - kwa maana ya wananchi kutofahamu athari zitokanazo. Mbaya zaidi, baadhi ya makampuni ya nje, badala ya kuzalisha mazao ya chakula, huamua kustawisha mazao yasiyo na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Kwa mfano, kustawisha mijatrofa, mitiiki/misaji, na pilipili hoho. Wilayani Kisarawe, kampuni iitwayo Sun Biofuel alimilikishwa hekta 8,210 kwa ajili ya kilimo cha jatrofa. 
Nini kifanyike 
Matatizo kama haya yanajirudiarudia nchi nzima. Mkuranga, Mvomero, Kilosa, Kilombero, Kiteto, Babati, Loliondo, Serengeti, Shinyanga, nakadhalika. Ni bomu linalosubiri kupasuka na kusababisha madhara makubwa ambayo yangeweza kuepukwa. Hivyo, kuna haja ya kuchukua tahadhari kabla bomu halijapasuka. Kwa hiyo, ACT inashauri ifuatavyo:
*  Ili kuondoa migongano katika matumizi ya ardhi, Serikali iandae Mpango wa Kitaifa wa 
    Matumizi ya Ardhi (National Land Use Plan). Aidha, iweke mipaka ambayo ni wazi na rasmi.  
    Mipaka hiyo iheshimiwe na wadau wote, vikiwemo vyombo vya Serikali. 

*  Wakulima na wafugaji waelimishwe kutambua ardhi iliyotengwa kwa matumizi yao. Vilevile, 
     watakaomilikishwa ardhi, wachukue jukumu la kuitunza na kuitumia vizuri, ikiwa ni pamoja 
     na kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti, na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

*  Sheria zinazohusu ardhi ambazo kwa sasa zinafanyiwa marekebisho, zitamke bayana kuwepo 
    kwa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kilimo na ufugaji. Aidha, ardhi hiyo itumiwe kwa ufanisi 
    kwa kuzingatia ikolojia, hali ya udongo, na mahitaji ya wakati huo.

*  Sheria na kanuni za ardhi zibainishe utaratibu wa kumiliki na kusimamia uendelezaji wa ardhi, 
     kwa kuzingatia madhumuni ya umilikishwaji wake. Kwa mfano: ardhi kwa ajili ya kilimo 
     isitumiwe vinginevyo bila sababu ya msingi. Endapo kuna mabadiliko ya lazima, vyombo 
     husika vijulishwe na viridhie.

*   Tabia ya kuhamahama ni miongoni mwa vyanzo vya kugombea ardhi. Iwekwe sheria ya 
     kudhibiti utamaduni huu. Wakulima na wafugaji wawe na makazi ya kudumu. Kuhamahama
     ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Mfano: mifugo kumomonyoa udongo, ukataji holela 
     wa miti, na uchomaji wa mkaa.

*   Utaratibu uliozoeleka ambao wawekezaji hupewa ardhi na vyombo vya juu kabisa bila 
     kushirikisha serikali za vijiji, mara nyingi hujenga uhasama usio wa lazima. Kwa hiyo, ni vema 
     kushirikisha ngazi za chini kuanzia wilaya, kata na vijiji husika. Kwani wenyeji wakielewa na 
     kuridhia, migogoro itapungua sana. 
     
*  Ardhi inayofaa kwa kilimo ipimwe, na wamiliki wapewe hatimiliki. Hii itakuwa na faida mbili. 
     Mosi, wakulima watakuwa na uhakika wa umiliki wa ardhi, hivyo kushawishika kuiendeleza 
     bila kusita. Pili, ardhi iliyopimwa na kupewa hatimiliki, ni dhamana tosha wakati wa kuomba 
     mikopo kutoka taasisi za kifedha.

*  Kuna haja ya kutoa huduma mahususi kwa wafugaji. Ardhi ya mifugo iwekewe miundombinu
     muhimu, kwa mfano mabwawa ya kunyweshea wanyama, majosho, na njia maalumu za 
     kufikia sehemu hizo. Aidha, wafugaji waelimishwe umuhimu wa kustawisha nyasi (malisho)
     kwa ajili ya mifugo yao. 

*  Endapo kuna haja ya kuchukua ardhi ya wakulima au wafugaji kwa manufaa ya umma, sharti 
    la kwanza waathirika waelimishwe kuhusu kusudio hili. Mchakato mzima uwe wazi. Aidha, 
    waanga wa zoezi hilo, sharti walipwe fidia stahiki.

*  La muhimu zaidi, ACT inasihi viongozi (hasa watendaji wakuu) wa vyombo vya Serikali 
    vinavyohusika, wajenge utamaduni wa kufika haraka katika maeneo ambayo yanaonyesha
    dalili za kulipuka kwa mzozo. Jukumu lao la kwanza ni kutuliza hali hiyo, pamoja na 
    kufanikisha suluhisho la kudumu. Ingawa sio rahisi kuridhisha kila mtu, lakini viongozi hao 
    wajitahidi kutenda haki kwa wahusika, bila kuegemea upande wowote.

No comments: