Pages

Tuesday, January 14, 2014

JAJI LIUNDI, HASHIM SAGGAF WAFARIKI DUNIA

Waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa Jaji, George Liundi nyumbani kwake, Keko jijini Dar es Salaam jana.  Jaji huyo anatarajiwa kuzikwa kwenye makaburi ya Chang'ombe keshokutwa.
Taifa limepoteza watu wawili mashuhuri. Hao ni Msajili wa Kwanza wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji George Liundi (78) na Mbunge wa zamani wa Dodoma Mjini, Hashim Saggaf.

Jaji Liundi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana alipokuwa akipelekwa Hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu wakati Saggaf, ambaye alikuwa Diwani wa Mtafukoge, Dar es Salaam alifariki jana saa nne asubuhi kwenye Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Saggaf alizikwa jana kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam na mazishi ya Jaji Liundi yamepangwa kufanyika keshokutwa.

Jaji Liundi
Jaji Liundi alikuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, mwaka mmoja baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, Julai mosi, 1993 na alistaafu mwaka 2001 na nafasi yake kuchukuliwa na John Tendwa ambaye naye alistaafu Agosti, mwaka jana na kumuachia kijiti, Jaji Francis Mutungi.

Wakati akiianza kazi hiyo, mfumo wa vyama vingi ulikuwa hauna nguvu, huku vyama vya siasa vikiwa vichache na kikubwa cha upinzani kilikuwa NCCR-Mageuzi.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, Keko Juu, Dar es Salaam, msemaji wa familia ambaye pia ni mtoto wa kwanza wa marehemu Liundi, Taji alisema baba yake kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo.

Alisema alikuwa yu mtu mwenye afya njema, lakini siku tatu zilizopita alikuwa akilalamika zaidi kuumwa mgongo.

“Afya yake ilikuwa nzuri licha ya kuwa alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu (BP), alikuwa akipatiwa matibabu kila alipokuwa akijisikia vibaya, kifupi alikuwa katika hali nzuri,” alisema Taji na kuongeza:

“Ijumaa na Jumamosi iliyopita nilimpeleka kwa daktari wake na kupatiwa matibabu. Jumapili (juzi) aliamka akiwa na afya nzuri,” alisema Taji.

Alisema hali ya Liundi ilibadilika ghafla usiku wa kuamkia jana, huku akiwa analalamika kuumwa mgongo... “Niliamua kumpeleka TMJ lakini tukiwa njiani, alifariki dunia.”

Taji alisema sasa wanasubiri ripoti ya madaktari, lakini wanaamini ugonjwa uliyomuua baba yao ni malaria kali. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
 
Alisema misa ya kumuombea Jaji Liundi itafanyika kwenye Kanisa Katoliki Chang’ombe wilayani Temeke, Alhamisi na mazishi yatafanyika katika Makaburi ya Chang’ombe.

Marehemu Liundi ameacha watoto watatu na mjane mmoja.

Jaji Liundi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1980.

Pia amefanya kazi katika nchi mbalimbali zikiwamo Zambia, Zimbabwe na Uswisi

Alikuwa mmoja wa Watanzania waliotengeneza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.”

Wanasiasa wamlilia

Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei alieleza kustushwa na taarifa za msiba huo na kusema anakumbuka ushirikiano wake kwa vyama vya siasa.

“Nawapa pole ndugu zake, watoto na mkewe kwa kumpoteza mtu muhimu, hiyo ndiyo njia tutakayopitia wote. Liundi alikuwa mtu mwadilifu nasikitika sana kusikia kifo chake,” alisema Mtei.

Kwa upande wake, Tendwa alisema Liundi anapaswa kuenziwa na Watanzania wote kwa kuasisi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi... “Watanzania wanatakiwa kumpa heshima kwa sababu yeye ndiye aliyeasisi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na michakato yote, zikiwamo sheria mbalimbali zilizopo hadi sasa.

“Yeye ndiye aliyesajili vyama vya awali vya upinzani mbali na CCM vikiwamo CUF, Chadema, TPP ambacho baadaye kilifutwa na vingine vingi. Alisimamia chaguzi za awali tangu mwaka 1994 hadi 1995. Alijitahidi kuubeba mfumo huo ukiwa bado mchanga… kimsingi yeye ndiye aliyetuwekea dira na kujenga msingi tulioukuta sisi, bila yeye tusingefika hapa tulipo.”

Nyuki wavuruga mazishi ya Saggaf
Waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya Saggaf walilazimika kukimbia kusaka hifadhi ya muda baada ya kundi kubwa la nyuki kuvamia eneo la makaburi saa kumi jioni.

Mtu mmoja, ambaye inaelezwa alikuwa na tatizo la kutoona vizuri alishambuliwa vikali na wadudu hao na kupelekwa Hospitali ya Regency kwa matibabu.

Hali ilitulia baada ya saa moja hivi na kutoa fursa ya shughuli za maziko kuendelea.

Mtoto wa marehemu, Ahmed Saggaf alisema baba yake alifariki baada ya kulazwa kwa siku tano kutokana na matatizo ya figo na ini.

Ahmed alisema kisomo cha kumuombea marehemu kitafanyika leo katika Msikiti wa Kipwata, Kariakoo, Dar es Salaam.

Saggaf alikuwa Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

No comments: