Pages

Friday, May 27, 2016

WANAHABARI WAMLILIA MAKONGORO OGING'

MAKONGORO
Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Publisher, Eric Shigongo (mwenye miwani) akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Makongoro Oging'.

NA NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM
WAANDISHI wa habari wa vyombo mbalimbali, jana walishindwa kujizuia wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa mwandishi wa Kampuni ya Global Publishers Ltd,  Makongoro Oging’ aliyefariki dunia Mei 21, mwaka huu.

Vilio na simanzi vilitawala katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Amana huku baadhi ya waandishi waliowahi kufanya kazi na mwandishi huyo wakianguka na kuzimia.

Makongoro anatajwa kuwa mmoja kati ya wanahabari nguli aliyeitumia vema kalamu yake katika kusaidia jamii  palipokuwa na tatizo na kuhabarisha umma.

Akizungumzia kifo hicho, Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Publisher, Eric Shigongo alisema msiba wa Makongoro ni pigo kubwa kwa kampuni yake na kwake pia.

Alisema Makongoro ni mmoja wa waaandishi aliyefanya naye kazi kwa miaka 15 bila kuonyesha dharau yoyote, aliipenda kazi yake na alikuwa mbunifu.

“Kwa ukweli taarifa yake ya msiba ilinishtua sana kwa sababu hakuumwa kwa muda mrefu, nilipokea taarifa zake za kuugua siku mbili kabla ya kifo chake na hapo nilihakikisha anapata vipimo vyenye uhakika kwa ajili ya kuimarisha afya yake lakini Mungu alimpenda zaidi,” alisema Shigongo.

Shigongo alisema marehemu alikuwa anasumbuliwa na malaria  na UTI lakini baada ya uchunguzi akabainika kuwa ana tatizo katika mapafu hali iliyosababisha kuumwa kifua.

“Msiba huu umenisikitisha sana kwa vile  hata kama watatokea waandishi wengine lakini bado pengo lake litabaki pale pale," alisema Shigongo.
Chanzo: Mtanzania Gazeti

No comments: