Pages

Friday, May 27, 2016

KILIO WAUZA BIA

beer

* Zuio la baa kufungwa mchana lazua balaa
* Mauzo TBL yashuka kwa asilimia 30

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
AGIZO la Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku kufungua baa wakati wa asubuhi limeanza kuporomosha mauzo ya bia zinazozalishwa na viwanda vya ndani.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo Machi 16, mwaka huu Ikulu Dar es Salaam baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa 26 aliowateua, huku pia akipiga marufuku mchezo wa pool table kwamba unawadumaza vijana na wanashindwa kufanya kazi.

Katika maagizo hayo, rais aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha baa zinafunguliwa saa 10 jioni na kufungwa saa 5 usiku.

Hata hivyo, agizo hilo la rais limegeuka mwiba kwa Kampuni ya TBL Group baada ya kushuka mauzo yake ya bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vyake kwa asilimia 30 kila mwezi jambo ambalo linatishia ustawi wa kiwanda pamoja na uchumi wa nchi.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano wa kampuni hiyo kueleza mchango wa bia katika uchumi wa taifa, Meneja mikakati wa TBL Group, Magabe Maasa, alisema kuzuia wafanyabiashara kufungua baa asubuhi kumepunguza mapato ya serikali.

Mkutano huo pia ulielezea utendaji wa kampuni hiyo kwa kipindi cha mwaka 2015 na mikakati ya kampuni kwa kipindi cha 2016/17.

Alisema ni vema serikali ipitie upya zuio hilo ili kunusuru uchumi kwa sababu hali ya mauzo ya bia kwa sasa ni mbaya tofauti na awali.

Maasa alisema kampuni yao inatengeneza ajira zaidi ya milioni mbili zikiwamo za moja kwa moja na zile zisizokuwa za moja kwa moja, hivyo kushuka kwa mauzo kunaathiri si mapato ya serikali tu bali pia ajira za Watanzania.

“Sekta ya vinywaji vyenye vileo imezalisha ajira zaidi ya milioni mbili za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja wakiwamo wakulima wa shayiri zaidi ya 3,000,” alisema.

Meneja huyo wa mikakati alisema serikali lazima iangalie mazingira ya sasa ni ya utandawazi ambapo si kila mtu anafanya kazi mchana pekee, huku akisisitiza kuwa baadhi ya watu hufanya kazi usiku na asubuhi huenda baa kupumzika huku shughuli nyingine zikiendelea.

“Tunaishauri serikali iangalie upya matamko yake, ikumbukwe kuwa kila chupa moja ya bia inayouzwa na TBL serikali inachukua asilimia 41 ya kodi, hivyo bia zisiponywewa hata yenyewe inakosa mapato yake kwa ajili ya kufanya miradi ya maendeleo,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Group, Roberto Jarrin, alisema kampuni yao inaongoza kwa ulipaji kodi ikiwa imechangia Sh trilioni 2.3 katika pato la serikali kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Mbali na hilo, alizungumzia hali ya biashara nchini ambapo alisema sekta ya vinywaji inakabiliwa na changamoto nyingi tofauti na mtazamo wa walio wengi.

Alisema hapa nchini bia zinauzwa bei ya juu ikilinganishwa na kipato cha kila siku kwa Mtanzania wa kawaida, huku akiitaja changamoto ya kutokuwepo kwa motisha katika uzalishaji wa malighafi zinazotumika kutengeneza bia nchini kwakuwa zinatozwa kodi kubwa ya zuio.

Jarrin alisema TBL Group pia inamiliki kiwanda cha Konyagi (TDL) na Chibuku (Dar Brew) huku ikizalisha na kuuza vinywaji vikali na baadhi ya pombe za asili kama Chibuku na Nzagamba.

Aidha, mkurugenzi huyo alisema wameamua kutengeneza vinywaji vya asili baada ya kugundua kuwa matumizi yake ni asilimia 50 ya pombe yote inayonywewa na kutengenezwa.

“Kampuni ya Dar Brew imeweza kuleta mapinduzi katika uuzaji wa pombe za asili kwa kuwezesha watumiaji kupata kinywaji cha Chibuku na Nzagamba katika mazingira ya usafi yanayolenga kulinda afya zao.

“Ipo haja kwa serikali kupunguza bei za vinywaji, hasa kwa upande wa bia ili kila mnywaji aweze kumudu kununua vinywaji kwani wengi wanashindwa kumudu na kuishia kuywa pombe haramu ya gongo ambayo haina ubora kwa afya ya binadamu,” alisema.

Alitolea mfano wa pato la Mtanzania kwa sasa kuwa halifiki Sh 5,000 kwa siku, lakini kinywaji kama bia huuzwa kati ya Sh 2,000 na 3,000 katika maeneo mbalimbali ya nchi.

WAFANYABIASHARA
Akizungumzia zuio hilo la   serikali, Donald Kavishe, ambaye ni Meneja wa baa maarufu ya Lubumbashi iliyoko Mbezi Mwisho jijini hapa, alisema tangu Rais Magufuli alipotoa agizo hilo Machi mwaka huu, biashara yake imekuwa ngumu kila kukicha tofauti na awali.

Alisema idadi kubwa ya wateja wake ni madereva wa bodaboda, bajaji na wale wanaoleta mizigo kutoka mikoani.

“Kama unavyoona baa yangu ipo karibu na kituo cha bodaboda na bajaji. Vijana wale walikuwa wanapenda kuja kunywa hapa kwangu wakati wakisubiri foleni ya kupakia abiria ifike.

“Lakini pia hapa jirani kuna soko, hivyo wale madereva wanaoleta mizigo kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wanakuja hapa kupata viburudisho wakati madalali walipokuwa wakishusha mizigo hiyo, lakini hivi sasa hawaji.

“Mauzo yangu yamepungua, kwa siku niliweza kuuza Sh 700,000 hadi Sh 800,000 lakini siku hizi nauza Sh 300,000 hadi 400,000,” alisema.

Kavishe alilalamika kulazimishwa kuuza vinywaji laini pekee kwa kuwa maofisa afya wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Luis hupita kukagua na iwapo mtu atakutwa akiwa anakunywa kinywaji chenye kilevi hutozwa faini ya Sh 50,000.

Aliiomba serikali iwaruhusu angalau kuuza bia moja hadi mbili kwa kuwa wapo wateja wengine huhitaji ili kutuliza mawazo.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa siku kadhaa umebaini baadhi ya wanywaji jijini Dar es Salaam huwaomba wenye baa kuwaficha kwa kuwafungia ndani ili kukwepa kukamatwa na serikali.

Baadhi ya baa hivi sasa zimetenga sehemu maalumu zenye uficho kwa wateja wanaohitaji huduma hizo kabla ya saa 10 jioni muda uliopangwa na serikali.

BIA ZA BEI CHEE
Aidha katika uchunguzi huo, MTANZANIA imebaini bia zenye ujazo mkubwa wa mil 500 zinakosa wateja tofauti na zamani.

Bia hizo ambazo huuzwa kati ya Sh 2,300 na 2,500 hivi sasa zimekosa soko baada ya kuwepo baadhi ya bia zinazouzwa kati ya Sh 1,500 na 1,700.

Mojawapo ya bia hizo ni Pilsner maarufu ‘Ukawa’ inayotengenezwa na Serengeti Breweries ya Dar es Salaam pamoja na bia ndogo ya Safari maarufu ‘emolo’ ambazo zinavutia wanywaji wengi kutokana na bei yake kuwa nafuu tofauti na nyingine.

WASEMAVYO VIJANA
Kijana Fred Halla ameliambia MTANZANIA kwamba ingawa agizo la serikali lilikuwa na nia nzuri ya kuwataka vijana kujishughulisha kiuchumi hata hivyo limewabagua.

“Rais Magufuli ameagiza baa zifunguliwe saa 10 jioni baada ya kazi, lakini wengi wanajua asubuhi hadi jioni ndio muda wa kazi jambo ambalo si kweli kwa sababu wapo wenzetu walinzi ambao tunajua muda wao wa kazi ni jioni hadi asubuhi.

“Kwa maana hiyo, binafsi naona agizo lile lina upungufu kwa sababu kuna matabaka mengi ya wafanyakazi na lazima wapewe haki kwa usawa.

“Kwa mfano mimi nipo likizo sasa hivi huwezi kusema sifanyi kazi,” alisema.

Alisema vijana wengi wanasikitishwa na agizo hilo kwani wakiwa kwenye vijiwe waliweza kukutana na wenzao wa sehemu mbalimbali na kupeana mipango ya kazi.

TRA
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alipoulizwa kama agizo hilo limeathiri makusanyo ya kodi, alisema kodi kwa kampuni kubwa kama TBL hesabu zake hupigwa kwa mwaka, hivyo hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.

“Hilo swali waulize wasambazaji na wenye baa wanaweza kukupa picha kamili ya mauzo yao kwa sasa, TRA sisi hesabu zetu zinakwenda kwa mwaka,” alisema Kayombo.

No comments: