Pages

Friday, May 27, 2016

DADA WA BILIONEA MSUYA AUAWA KINYAMA DAR


Anathe Msuya
Marehemu Anathe Msuya, enzi za uhai wake.

DADA wa marehemu Erasto Msuya aliyetambuka kwa jina la Anathe Msuya, ameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Dar es Salaam.

Anathe aliuawa nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni, ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya nyumba yake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kuahidi kutoa taarifa kamili leo.

“Ni kweli kuna tukio hilo la kifo, lakini taarifa kamili kwa undani nitazitoa kesho (leo), ninaomba muwe na subira,” alisema Kamanda Sirro.

Anathe ni dada wa marehemu Erasto Msuya ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite aliyeuawa kwa kufyatuliwa risasi.

Msuya aliuawa Julai 7, mwaka 2013 katika eneo la Mijohoroni,  kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, akiwa ameitika wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite baada ya kupigiwa simu na vijana wawili  waliomtaka wakutane maeneo hayo.

Inaelezwa kuwa alifika katika eneo hilo akiwa na gari lake aina ya Range Rover T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri.

Baada ya kuteremka,  Msuya aliekea kumsalimia mmoja wa vijana hao, hata hivyo kabla hajamfikia kijana huyo aliitoa bunduki ya SMG namba KJ 10520 aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi takribani 22 mwilini.

Bilionea huyo aliyekuwa akimilika vitega uchumi mbalimbali jijini hapa na maeneo mengine nchini aliuawa saa 6:30 mchana.

Taarifa za polisi zilisema katika eneo la tukio ilikutwa  bastola  namba GLS 417T2 CAR 83271, mali ya Msuya na vitu vingine, ambavyo ni simu ya Samsung S5, iPhone na koti la mmoja wa watuhumiwa likiwa limetelekezwa mita chache kutoka eneo la tukio.

Polisi waliweza kuwakamata watuhumiwa wa mauaji hayo na kuwafikisha mahakamani mjini Moshi ambako kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.
Marehemu Anathe Msuya enzi za uhai wake akiwa na mwanae Allan.

Nyumba ya marehemu Anathe Msuya iliyopo Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam.

Marehemu Anathe Msuya, enzi za uhai wake.
Chanzo: Mtanzania Gazeti

No comments: