Uongozi wa Young Africans ya Dar es Salaam, umekamilisha
maandalizi yote muhimu ya mchezo dhidi ya GD Sagrada Esperanca ya Angola
wa kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho la Barani Afrika
utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho Jumamosi Mei 7, saa
10:00 jioni.
Mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana ukisimamiwa na kamishna kutoka Ethiopia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ametaja viingilio vya mchezo huo kuwa
Jukwaa la VIP “A” kuwa ni Sh 30,000; VIP “B” na “C” Sh 20,000 wakati
jukwaa la viti Rangi ya chungwa ni Sh 7,000 wakati mzunguko wa viti vya
bluu na kijani ni Sh 5,000.
Kwa mujibu wa Muro, Yanga itawakosa wachezaji mahiri wawili,
Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao watatumia mchezo huo kutumikia
adhabu ya kadi mbili za njano walizoonywa kwenye michuano ya Ligi ya
Mabingwa Afrika kabla ya kushuka kucheza Kombe la Shirikisho.
“Tunawaomba wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga
tujitokeze kwa wingi kesho kuishangilia timu yetu kwa nguvu na kasi
kubwa,” amesema Muro ambaye alitumia nafasi hiyo kutamba kwamba Yanga
ilisajili wachezaji 24 kwenye michuano inayoratibiwa na Shirikisho la
Soka Barani Afrika (CAF).
No comments:
Post a Comment