Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na wWatoto inasikitishwa na
inalaani vikali tukio la kuuawa kwa kuchinjwa, mwanamke Oliver Erasto
(23) na mtoto wake Emmanuel (3), wakazi wa eneo la Zinga, kata ya Dunda,
wilayani Bagamoyo, kutokana na wivu wa kimapenzi.
Wizara inakemea maauji hayo,
yanayodaiwa kufanywa na Frowin Mbwale mkazi wa Kawe, Dar es Salaam,
ambaye ni mume wa marehemu, kwani yamesababisha kukatisha maisha ya mama
na mtoto, katika kipindi ambacho taifa linahimiza uzingatiaji wa mchango
na haki za wanawake katika maendeleo ya taifa, na mwitikio wa haki ya
kuishi ya mtoto katika mipango na programu za maendeleo endelevu.
Wizara inasisitiza kutambua kuwa
jukumu la ulinzi na usalama wa wanafamilia liko mikononi mwa kila
mwananchi, hivyo jamii inawajibu wa kusaidia udhibiti wa ukatili na
mauaji katika familia na jamii zetu.
Jamii ikiwa na uelewa wa pamoja
katika haki za wanawake na watoto katika jamii, itawezesha kuwekeza
katika haki ya kuishi ya mtoto, na kuendelea kuwaamini wanawake kwamba
wanaweza kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza familia zao, na taifa
likaweza kupiga hatua kufikia maendeleo endelevu.
Wizara inapenda kulipongeza Jeshi la Polisi
mkoa wa Pwani na wananchi walitoa taarifa zilizowezesha watuhumiwa wa
mauaji haya kukamatwa, na tunaamini kuwa watakapofikishwa mbele ya vyombo vya
sheria haki itaweza kutendeka.
Wizara inapenda kutoa pole kwa
familia za marehemu hao waliopoteza maisha kwa kuchinjwa na kuawa, na
kuwaombea kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha majonzi
makubwa.
Wizara inaitaka jamii itambue kuwa hakuna mwenye haki ya
kukatisha uhai wa mtu mwingine, na mwanamke na mtoto wana haki ya
kuthaminiwa utu wao, bila ubaguzi wowote ambao unaweza kukatisha maisha
yao.
Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
No comments:
Post a Comment