![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. |
Ndugu Wananchi;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na
kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila
mwisho wa mwezi. Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza nanyi.
Ziara ya Rais wa China Nchini Tanzania
Ndugu
wananchi;
Jambo la kwanza ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa
Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi,
2013. Lengo la ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati
ya China na Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wakazi wa Dar es
Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe wake. Wameondoka wakiwa na
kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na watu wake.
Kwa niaba yenu, nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi
Jinping akielezea kufurahishwa na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba
tuendelee kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri
watakaotutembelea siku za usoni.
Ndugu wananchi;
Nami pia, nimemshukuru sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali
mwaliko wangu na kufanya ziara ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi
yetu. Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa na kumbukumbu
isiyosahaulika. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena
siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake. Na, kubwa zaidi ni
kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya China kwa
Afrika katika kipindi cha uongozi wake.
Tumefarijika sana kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa
kipaumbele cha juu na viongozi wapya wa China. Pia, kuwa China itaendelea
kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika ikiwemo
kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika. Kama mtakumbuka nchi
zetu mbili zilitiliana saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja
mbalimbali. Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya kipaumbele nayo
imejumuishwa.
Ndugu Wananchi;
Rais Xi Jinping alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali
na Chama cha Kikomunisti cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo
kati ya Tanzania na China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na
waasisi wa nchi zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa
kwanza wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na
Waziri Mkuu wake Chou En Lai.
Rais wa China aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na
Tanzania katika medani ya kimataifa na kuchangia katika jitihada zetu za
kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada ya maendeleo. Katika miaka 49 ya
uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo
ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa na
Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.
Ndugu wananchi;
Kuna miradi kadhaa mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na
Zanzibar, kwa msaada wa Serikali ya China. Wakati wa ziara yake, Rais Xi
Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama
tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku
ile.
Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa
Jijini Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka
kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa katika jiji la Dar es
Salaam. Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na
simanzi kubwa nchini. Mpaka sasa maiti za ndugu zetu 30 zimepatikana.
Watu 17 waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado wanaendelea na
matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Wengine walitibiwa na
kuruhusiwa. Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na sasa inakaribia kufikia
ukingoni.
Ndugu Wananchi;
Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia
eneo la ajali. Hali niliyoiona pale imenihuzunisha sana. Lazima nikiri, hata
hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa
zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na
wananchi. Napenda kutumia nafasi kutoa shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa uongozi wake madhubuti. Pia nampongeza
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na
wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za
uokoaji.
Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya
waliojeruhiwa. Nawapa pole wale wote waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao
katika ajali hii. Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote tukiungana nao
kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi. Kwa waliojeruhiwa,
tunawaombea wapone upesi.
Ndugu Wananchi;
Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile. Alimradi
kila mtu ana dhana yake. Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue hatua
zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika
kusababisha maafa hayo wachukuliwe hatua zipasazo. Wa kushtakiwa Mahakamani
washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao
wafutiwe bila ajizi. Jambo la msingi la kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika
na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize ipasavyo wajibu wake. Naamini kama
mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika.
Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu maalum kwenye ujenzi katika maeneo
yao. Watimize wajibu wao. Yaliyotokea Dar es Salaam yawe fundisho kwa
wote.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na Bodi
ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli
ujulikane. Bodi ya Usajili wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi na
Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe kwa ukamilifu ili ukweli upatikane
na hatua stahiki zichukuliwe. Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha ajali
za aina hiyo siku za usoni.
Uhusiano wa Wakristo na Waislamu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano wa
Waislamu na Wakristo nchini. Jambo hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za
nyuma, lakini nalazimika kulisemea tena kutokana na hali ilivyo sasa. Tumefikia
mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa mbili hawatakubali
kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya. Nchi yetu nzuri tutaivuruga
na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa
upendo, ushirikiano na kuvumiliana itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha
amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita vya wenyewe
kwa wenyewe.
Ndugu Wananchi;
Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za
Kikristo na Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli
hizo zina mambo mawili makuu. Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu
na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli
na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu,
kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi
wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.
Na, pili kwamba kila upande unailamu Serikali kwa kupendelea upande
mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo
inaendeshwa na Serikali haichukui hatua. Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi
wao kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua. Kwa ajili hiyo wanadai
kuwa Serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba
Serikali inapendelea upande wa Waislamu.
Ndugu Wananchi;
Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu,
kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na
Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi
yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea
Wakristo. Wanasema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi
wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi kwenye shughuli za Wakristo kuliko
za Waislamu kama vile harambee za kujenga Makanisa na shule za Makanisa.
Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki.
Ipo Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife. Katika itikafu
hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi
wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman
Kova.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na
Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote. Hatufurahishwi na kitendo
cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya
Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa
nyakati mbalimbali. Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wake huo na kama
haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni
sera na maelekezo yangu au ya Serikali. Mtakumbuka kuwa mara kadhaa
nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha
ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.
Ndugu Wananchi;
Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila
ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo. Nimeshafanya shughuli
nyingi za Waislamu kama vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija,
ujenzi wa misikiti na madrasa na mengineyo mengi. Nimeshashiriki mazishi ya
Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo.
Pale ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya
kubanwa na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya
muda mfupi. Kwa upande wa Waislamu desturi yetu ya kuzika mara mtu anapofariki
huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya
taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo
nyepesi. Wakristo hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia
rahisi kushiriki.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda
usalama wa raia wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada. Kama ingekuwa
hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa
nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini. Lakini hivyo sivyo. Nawasihi sana
ndugu zangu Wakristo na Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa
Mchungaji Mathayo Kachila kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule
Zanzibar, au kumwagiwa tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar,
kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na
Mbagala, Dar es Salaam kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa
kutimiza wajibu wake.
Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya
Serikali kuzembea. Hakuna ushahidi wa matukio hayo kuunganika. Mpaka sasa
hatujapata ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa
Kikristo na kuchoma moto Makanisa hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu
zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini
ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu. Katika ugomvi na
vurumai hizo ndipo watu kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza
maisha. Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo nchini. Ni la pale pale
Buseresere na limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa
sababu zao.
Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile
kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na
Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao. Walikuwa wanaishi kidugu
na kushirikiana katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja
akimuabudu Mungu kwa misingi ya dini yake. Hivyo kutumia tukio hilo kutoa wito
kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni sawa na kuuawa kwa
Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza tatizo isivyostahili.
Busara ituongoze kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa
Buseresere wazungumze, waelewane na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa
awali. Hata mzozo wa kuchinja wanaweza kuumaliza. Mbona bucha za kitimoto zipo
na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya Wakristo
na Waislamu nchi nzima si sawa. Hatuwatendei haki Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio
linalojitegemea halina uhusiano kabisa na lile la Buseresere, Geita. Hapakuwa
na mzozo kuhusu nani achinje. Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha
vyombo vya upelelezi vya nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi. Tumefanya
hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa matukio ya kabla
yake. Yaani ile la kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na
kumwagiwa tindikali kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga. Bado
hakuna mafanikio ya kutia moyo. Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu
yanahusiana. Je, Makanisa kuchomwa moto kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote
na matukio yale matatu? Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo
hilo.
Kuna watu wanadhani yanahusiana na kwa sababu nzuri. Lakini inabaki
kuwa ni dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika. Bado kazi ya
uchunguzi inaendelea kufanywa na vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana
na wenzao wa nje. Katika mazingira hayo, ni mapema mno kumnyooshea kidole mtu
ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Serikali siyo mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya
kufanya hivyo. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana kupata
jawabu.
Ndugu Wananchi;
Hali kadhalika tukio la Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa,
kubomolewa, mali kuibiwa na kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina
mazingira yake maalum. Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la kusikitisha
la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu, yaani Quran
Tukufu. Pamoja na maelezo kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake,
lakini kitendo hicho kiliwakasirisha Waislamu. Kijana huyo alifikishwa kituo
cha Polisi. Baadhi ya Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo
wakidai wapewe huyo kijana wamuadhibu wao. Jeshi la Polisi lilikataa.
Kukatokea mzozo kati ya waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa
walichokitaka baadhi yao walipotoka pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja,
kuiba na kuchoma moto Makanisa.
Ndugu Wananchi;
Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa
mahali popote kwa upande wa Bara. Aidha, hapajawahi kuwepo tishio
lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote. Lakini maneno ya vitisho
vya kuchoma Makanisa yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi. Kila
ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa
na hata hatua za tahadhari kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja
iliyothibitika kuwa na chembe ya ukweli. Hata dalili
hazijakuwepo.
Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali
hupelekwa kote, kwa Wakristo na Waislamu. Upo unaowalenga Wakristo ukiwaambia
wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru. Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa
Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. Watanzania wenzangu nawaomba
mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza mchezo mchafu wa kuwagonganisha na
kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu kwa sababu wanazozijua wao na kwa
faida yao. Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu
wagombane. Wanapandikiza chuki baina ya Serikali na waumini wa dini zetu kuu
mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza raia wake. Ni mchezo mbaya,
tusikubali kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza
kumetokea nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na
Waislamu na kutishia kuleta vita baina nchini kote?
Ndugu Wananchi;
Serikali haijapuuzia kila palipotokea matukio ya uhalifu.
Watu 76wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na
kufanya fujo kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani.
Kwa upande wa tukio la Buseresere lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo
Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu
walikamatwa na kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo
walioshitakiwa kwa kufanya vurugu. Jeshi la Polisi bado linawatafuta watu
wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa upande wa Zanzibar,
watu 10 wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao
zinaendelea. Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la kuchoma Kanisa baada
ya kuuawa Padri Evaristus Mushi. Uchunguzi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi
haujakamilika pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi.
Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi, baada ya jitihada kubwa kufanyika
ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea katika uchunguzi wa makosa ya
aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa. Mtu mmoja amekamatwa na wengine
wanaendelea kutafutwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua
hatua. Watu kadhaa wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani katika maeneo
mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na kusambaza kanda zinazochochea chuki na
vurugu za kidini. Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine ambao
wanaendelea kutafutwa. Zipo taarifa kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje.
Jeshi la Polisi limeomba msaada wa Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia
kuwatafuta na kuwarejesha nchini. Vituo viwili vya radio yaani Kwa Neema FM cha
Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa miezi sita. Baada
ya muda huo kupita, Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua
ipasavyo.
Ndugu Wananchi;
Nimeyaeleza haya kwa kirefu kuwahakikishia kuwa Serikali inajali
usalama wa raia wake wa mali zao na amani na utulivu wa nchi yetu. Kamwe
hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na
yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila yote,
rangi zote na mahali po pote walipo wako salama. Tunataka kuona watu
wanaendelea kuishi kwa amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa
tunaishi siku zote. Tunapenda kuona Watanzania wanaepuka mambo yanayowabagua na
kusisitiza yale yanayowaunganisha. Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale
yanayotugawa.
Ndugu Wananchi;
Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho kwetu
sote. Tuazimie sote kuwa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Hebu tufikirie
maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za kijamii kama vile sherehe,
harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na chakula tofauti kwa Waislamu na
Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali, shule na vyuo pawe na majiko
mawili au labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini
nako kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo. Hali iwe hivyo hivyo
kwenye migahawa na maeneo mengine yenye huduma ya chakula.
Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi
ya namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa
kubaguana kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo
hatutakuwa wamoja tena. Huko tunakoelekea siko, ni kubaya. Tubadilike, na
wakati ni huu. Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa
letu na janga hili.
Ndugu Wananchi;
Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu kubwa
mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi. Ni wao kuliko mtu
mwingine ye yote wenye majawabu ya matatizo haya. Ni masuala yanayohusu imani
za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa jina la dini zao.
Serikali ina wajibu wa kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini
hawatafanya vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini
lipi jema na lipi baya ni viongozi wa dini.
Ndugu Wananchi;
Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa madhehebu na taasisi za dini za
Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu jambo hilo. Nimepata faraja kuona
kuwa wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya
viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza. Wanakiri kuwa
hali ilivyo sasa siyo ya kawaida kwa Tanzania na Watanzania. Kuna upepo mbaya
wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa kuhakikisha kuwa hali
ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake katika maisha
tuliyoyazoea. Maisha ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu,
upendo, ushirikiano na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania
wao.
Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya
Serikali ya kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao. Ni
matumaini yangu kuwa wote watashiriki wenyewe bila ya kutuma wawakilishi.
Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na
kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita
vya kidini. Waache kushabikia taarifa zinazochochea na kujenga uhasama baina ya
waumini wa dini zetu. Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla ya kuziandika
au kuzitangaza. Wawe makini na maneno wanayotumia. Katika hali tuliyonayo sasa
lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga umoja miongoni mwa
Watanzania wa dini zote. Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro
mkubwa ambao hauna msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani. Nawaomba
wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa kuhakikisha vyombo
vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama baina ya Wakristo na
Waislamu.
HITIMISHO
Ndugu Wananchi;
Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote kudumisha
umoja na mshikamano wetu. Tuishi kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano
bila kujali tofauti ya dini zetu, kabila, rangi au mahali atokako mtu. Hizo
ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi, kuzilinda na
kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini yo yote na
wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini wao. Serikali
kupitia vyombo vyake vya usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa
raia wake na mali zao kama inavyofanya siku zote. Kama kuna mtu anaona kuwa
maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa Polisi. Hatua
zipasazo zitachukuliwa.
Ndugu Wananchi;
Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka. Tusherehekee kwa amani na
utulivu. Tusherehekee pamoja.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
1 comment:
Inaridhisha kiasi fulani.......
Post a Comment