Pages

Tuesday, March 5, 2013

SAIGON PUB MABINGWA MASHINDANO YA NYAMA CHOMA - MBEYA

 Majaji wa shindano hilo wakiongozwa na jaji mkuu, Douglas Sakibu (katikati).

Jiko la baa ya Nebana ambao wameibuka washindi wa nne.

Jiko la baa ya Chabruma ambao waliibuka washindi wa tano.

Jiko la Saigon Pub wakikata nyama tayari kwa kuliwa.  Wao ndio waliibuka
washindi katika mashindano hayo.

 Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispin Meela akikagua majiko wakati wa
mashindano hayo.

 Bendi ikitumbuiza katika mashindano hayo.

 Mpishi mkuu wa Saigon Pub ambao ndio waliibuka kidedea katika mashindano hayo,
akipokea zawadi na cheti kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Rungwe, Bw. Meela.

Meneja wa baa ya Mbeya Carnival, ambao ni washndi wa tatu akipokea
fedha ya zawadi kutoka kwa mkuu wa wilaya ya Rungwe, Bw. Meela.
(Picha zote na Shabani Tolle)

Na Mwandishi Wetu

SAIGON Pub, wametwaa ubingwa wa mashindano ya Nyama Choma Mkoa wa Mbeya, baada ya kuzishinda baa nyingine nne (4) zilizotinga fainali ya mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Safari Lager.

Fainali za mashindano hayo zilifanyika juzi Jumapili kwenye uwanja wa CCM Ilomba ambapo washindi hao walizawadiwa fedha taslim Shilingi milioni moja pamoja na cheti.

Washindi wa pili walikuwa New City Pub ambao walizawadiwa Sh. 800,000 na cheti, wakifuatiwa na Mbeya Carnival waliotwaa ushindi wa tatu na kuzawadiwa kitita cha Sh. 600,000 na cheti.

Washindi wengine ni baa ya Nebana ambao walichukua nafasi ya nne na kuibuka na Sh. 400,000 na cheti, wakati baa ya Chabruma ilishika nafasi ya tano na kuzawadiwa Sh 200,000 na cheti.

Akizungumza kabla ya kumtangaza mshindi, Jaji Mkuu wa fainali hizo, Douglas Sakibu, alisema kuwa walitoa mafunzo kwa baa zote hizo juu ya mambo wanayopaswa kuzingatia katika uchomaji nyama ambapo alivitaja vigezo walivyotumia kupata mshindi kuwa ni usafi wa mchomaji, vifaa na mazingira, maandalizi ya nyama kuanzia uchaguzi, uhifadhi wake na wa vifaa.

Vingine ni uchomaji na upangaji nyama, ladha na ulaini wake, mazingira ya eneo, mtiririko wa maji na uhifadhi wa taka.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa Bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo, alisema kuwa ni fahari kubwa kwa TBL na bia ya Safari Lager kwa ujumla kufanikisha shindano hilo mkoani hapa kabla ya kuhamia mikoa mingine.

“Tulianza kwa kuwataka watu wapige kura kupendekeza baa zinazofaa kuingia katika shindano la nyama choma kwa mkoa huu wa Mbeya tukapata baa hizi tano zilizoingia fainali ambapo leo tutampata mshindi.

“Tunajua watu huwa wanakwenda katika baa na kula nyama hivyo tukaona ni vema tuanzishe mashindano haya ili walaji nyama choma wapate nyama bora,” alisema.

Alisema kuwa bia ya Safari Lager ina miaka takriani 36 na bado imeendelea kuwapo hadi sasa ambapo Mbeya ndio inayoongoza kwa mauzo ya bia hiyo miongoni mwa mikoa yoye ya Tanzania.

Kwa upande wake, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela, aliisifu TBL kupitia Safari Lager kwa kuandaa mashindano hayo, akisema kuwa serikali inatambua mchango wa kampuni hiyo katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia tukio hilo na mengineyo kama mashindano ya Pool Safari Lager, Safari Wezesha na hata udhamini wao katika michezo mbalimbali kama soka na mingineyo.

“Mashindano haya ni mazuri kwani yanawajengea wateja wa nyama mazingira mazuri na salama katika kutoa huduma hii ya nyama choma,” alisema.

Alizitaka baa ambazo hazikufika fainali, kutokata tamaa na badala yake kujipanga kwa ajili ya mashindano ya mwakani, kwa kurekebisha yale waliyokosea mwaka huu.

No comments: