Pages

Tuesday, March 5, 2013

HADI SASA UHURU KENYATTA AONGOZA

Uhuru Kenyatta, mgombea urais Kenya.
Raila Odinga, mgombea urais Kenya

Matokeo ya awali ya kura za uchaguzi wa urais nchini Kenya, yaliyotolewa karibuni kutoka kwa tume ya uchaguzi yanaonyesha kuwa Raila Odinga ana kura 2,133,202 wakati Uhuru Kenyatta ana kura 2, 718,021.

Hadi kufikia saa 12.00 jioni matokeo yalikuwa yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta anaongoza dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga licha ya matokeo kutoka sehemu mbali mbali kuchelewa hasa kwa sababu ya hitilafu za kimitambo.

Wakati huo huo zaidi ya kura laki mbili inasemekana zimeharibika kutokana na sababu mbalimbali.  Kura kura hizo ni karibu mara mbili ya kura alizopata mgombea wa urais wa muungano wa Amani, Musalia Mudavadi zikijumulishwa na kura walizopata wagombea wengine waliokuwa na kura chache zaidi.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, imesema ina wasi wasi kuhusu idadi ya kura zilizoharibika na imesema italazimika kuchunguza kisa cha idadi kubwa ya kura kuharibika.  Wamesema kuwa sababu ya kuharibika kwa kura itatolewa baada ya uchunguzi kamili kufanywa pamoja na maoni ya maafisa waliosimamia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Ahmed Issack Hassan, amesema kuwa uchunguzi utafanywa mwishoni mwa uchaguzi kujua kwa nini wapiga kura walifanya makosa makubwa wakati wa upigaji kura.

''Ni kweli hii ni idadi kubwa sana ya kura zilizoharibika,''alisema bwana Hassan.  Hizi ndizo kura zilizopigwa na ambazo sasa zimeharibika, aidha kwa sababu ziliwekwa alama isiyostahili.'' alisema Hassan.

Wakati wa shughuli hiyo tume iligunduwa kuwa kuna mahali ambapo wapigha kura waliweka karatasi za kura katika masunduku yasiyostahili.

Bwana Hassan alisema kuwa huenda rangi ziliwachanganya watu kwani hazikuwa na nguvu sana, kama mfano rangi ya kijani kibichi haikuwa kama ilivyostahili kuwa.

Aliongeza kuwa huenda tatizo hili linatokana na ugumu wa upigaji kura ambapo wapiga kura walikuwa wanachagua wagombea sita wakiwemo, wabunge, waakilishi wa wanawake, maseneta, magavana, wawakilishi wa wodi na Rais.

Source:  www.bbc.co.uk/swahili

No comments: