Pages

Thursday, February 21, 2013

MANISPAA YA TEMEKE YAANZA KAMPENI YA USAFI

(Na Shabani Tolle)
Manispaa ya Temeke imeanza utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhaji Said Meck Sadiki la kuhakikisha kuwa jiji la Dar es Salaam linakuwa safi kwa kuanzisha operesheni maalumu ya kuwakamata wachafuzi wa mazingira.
Zoezi hilo linawahusu wanaochafua mazingira kwa makusudi, wafanyabiashara waliopo katika maeneo yasiyo rasmi na wanaotiririsha maji machafu ambapo wahusika watapigwa faini na wengine kuwafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Afisa afya wa manispaa hiyo bi Rehema Sadiki amesema kuwa kampeni hiyo itakuwa endelevu na kwamba watu wote watakaokamatwa watalazimika kulipa faini ya kuanzia shilingi elfu 20 mpaka elfu 50 kulingana na kosa ambalo atakamatwa nalo mhusika.
”Tumeanza kampeni hii katika maeneo ya usoni kwa kuwakamata wale wote wanaofanya biashara zisizo rasmi kandokando mwa barabara pamoja na mama lishe marufu kama mama ntilie” amesema.
Naye mkuu wa operesheni hiyo Bw Jeremiah Munuo amesema zoezi hilo litakuwa likifanyika kila Jumanne na Alhamisi na kwamba mpaka sasa wameshawakamata watu zaidi ya 150 na kuwatoza faini ya zaidi ya shilingi milioni 1.
“Awamu ya pili tutahakikisha tunawakamata wale wote wa majumbani wanaotiririsha maji machafu kwa wenzao na bararabarani na ambao vyoo vyao vimejaa na hawataki kuvuta” amesema.
Aidha Bw. Munuo ameitaka jamii hususani wanaoishi katika manispaa ya Temeke kuhakikisha kuwa wanaachana na tabia ya kuchafua mazingira jambo ambalo limekuwa likisababisha kutokea kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo ugonjwa hatari wa kipindupindu ambao umekuwa ukiuwa idadi kubwa ya watu.
Mama Gaudiana Ntego ambaye ni mwenyekiti wa umoja wa mama lishe eneo la Tazara ameongelea umuhimu wa zoezi hilo ambapo amefafanua kuwa ni muda mrefu sasa mabwana afya hawajapita katika maeneo yao na amewashauri wawe wanapita mara kwa mara katika maeneo yao ili wawaelimishe na kuwakumbusha masuala mbalimbali ya afya.
“Napongeza zoezi hili kwa kuwa linatukumbusha masuala ya afya.  Mtu akipigwa faini ya shilingi elfu ishirini au elfu hamsini inamuuma na itamfanya asirudie kosa sababu mimi ninajitahidi sana kuwaelimisha kuhusu masuala ya afya, wakati mwingine wananidharau ila sasa wameona wenyewe kilichowapata” mama Gaudiana alisema.
Manispaa  hiyo imeanzisha zoezi hilo kufuatia jiji la Dar es Salaam kukithiri kwa uchafu jambo ambalo lilimpasa mkuu wa mkoa kuwaita watendaji wa manispaa zote na kutoa mwezi mmoja kuhakikisha jiji la Dar e es salaam linakuwa safi kwa mujibu wa sheria.

Pichani baadhi ya mama/baba lishe waliokamatwa maeneo ya soko la Tazara, DSM
(Picha na Shabani Tolle)

No comments: