Pages

Tuesday, April 19, 2022

COSTECH YAMTEMBELEA KIPANYA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt Amos Nungu (wa kwanza kulia) akiendelea na mazungumzo na Mbunifu wa gari la umeme wa Kaypee Motors Ltd, Masoud Kipanya (mwenye Tshirt nyeusi)  akiongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji Teknolojia, Dkt Erasto Mlyuka (watatu kushoto) na Afisa Uhusiano kutoka COSTECH Bw. Faisal Abdul (wakwanza kushoto) wakati wa ziara fupi ya Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group iliyofanyika jana Mikocheni Jijini Dar es salaam.

Mbunifu Masoud wa Kaypee Motors Ltd (wakwanza Kulia) akishauriana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt Amos Nungu (wa pili kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji Teknolojia, Dkt Erasto Mlyuka mara baada ya kukagua gari la umeme  wakati wa ziara fupi ya Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group iliyofanyika  jana Mikocheni Jijini Dar es salaam.

Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH akiambatana na wataalam wa ndani ya Tume hiyo  wakati wa ziara fupi ya Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group iliyofanyika jana Mikocheni Jijini Dar es salaam.

Na Faisal A. Jalil, COSTECH,

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt Amos Nungu amefanya ziara fupi katika Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group kilichopo mikocheni jijini Dar es Salaam kumtembelea mbunifu Bw. Masoud Kipanya wa Kaypee Motors Ltd kutokana na ubunifu wake alioutangaza hivi karibuni kutengeneza gari linalotumia umeme.

Katika mazungumzo yao, Dkt. Nungu alisema kuwa Serikali kupitia COSTECH imekuwa ikiwahudumia wabunifu mbalimbali kwa ushauri, ufadhili wa fedha, na hata kuwaunganisha na Taasisi mbalimbali za Serikali na vyuo vikuu ili kuwezesha wabunifu hao kufikia ndoto zao.

Alifafanua kuwa tangu aingie COSTECH mwaka 2018, Serikali imeweza kutoa zaidi ya Tsh. Milioni 200 kuwawezesha wabunifu wa magari pekee nchini ili kuboresha bidhaa mbalimbali za kibunifu walizokuwa nazo.

“Kazi kubwa ya Serikali ni kuweka mazingira na miundombinu wezeshi, tumekutemebela rasmi ili kujua mipango yako, na mahitaji yako halisia ambayo ungetamani Serikali ikutimizie kupitia COSTECH”,alisema Dkt. Nungu

” Tunatamani kujenga au kufadhili taasisi na mifumo ambayo itasaidia kufanya kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa utengenezaji wa magari, vipuli mbalimbali vya gari la KayPee Motors Ltd viweze kuzalishwa hapa nchini”, aliongeza Dkt. Nungu.

Kwa upande wake mbunifu Masoud Kipaya kupitia kampuni ya Kaypee Motors aliishukuru Serikali kupitia COSTECH kwa kumfikia na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa za kibunifu za ndani zinazalishwa kwa wingi nchini kupitia kazi za wabunifu mbalimbali.

Mbunifu Masoud ameahidi kutoa mahitaji yake halisi ndani ya siku mbili zijazo ili COSTECH iweze kuyatathmini na kutoa usaidizi stahiki. 

 

 

 

 

No comments: