Pages

Wednesday, July 7, 2021

NAIBU WAZIRI MHE MWANAIDI ATAKA MIRADI YA UBUNIFU CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII RUNGEMBA

 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amewataka wanafunzi katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba kubuni miradi mbalimbali kutokana na mazingira  yanayowazunguka ili kujinufaisha na jamii zao.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema hayo katika Ziara yake Chuoni hapo ya kukukagua shughuli zinazoendeshwa ikiwa ni pamoja kilimo cha parachichi na shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Aidha, ameeleza kuridhishwa kwake na shughuli mbalimbali zinazoendeshwa Chuoni hapo na kuwataka wanachuo kuongeza bidii na maarifa ili shughuli wanazozifanya zikidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akiwa Chuoni hapo, Naibu Waziri Mwanaidi amezindua vyumba viwili vya madarasa vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila kimoja pamoja na Kituo cha Kidigitali cha ubunifu na maarifa.

Kupitia ziara hiyo, ametembelea shamba darasa la miparachichi linaloendeshwa na wanafunzi wa chuo hicho na baadaye kukagua Shamba la mmoja wa wakulima wa zao hilo ambalo limeelezwa kustawi zaidi katika eneo la Mufindi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameeleza kufurahishwa na juhudi za Serikali kukiwezesha Chuo hicho kuendesha shughuli za ubunifu ambazo zinawanufaisha vijiji vinavyokizunguka chuo.

Akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba, Kidubya Kulamiwa ameishukuru Wizara kwa kutenga fedha za uendeshaji wa Chuo na kuziwasilisha kwa wakati.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saadi Mtambule amepongeza Wizara ya Afya kwa programu za ubunifu ambazo zimeleta manufaa kwa jamii.

Mtambule ameahidi kwamba Serikali katika ngazi ya Wilaya itahakikisha inaweka mpango na ufuatiliaji wa mipango iliyopo kuhakikisha Chuo kinafanikisha malengo ya kuwakwamua watanzania dhidi ya changamoto mbalimbali za maisha.

Awali, Naibu Waziri Mwanaidi alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga Ofisini kwake na kufanya mazungumzo kuhusu hatua mbalimbali za maendeleo Mkoani humo.

No comments: