Waziri wa Nishati Dk .Merdard
Kalemani ,akizungumza na baadhi ya wananchi,viongozi na wafanyakazi wa
kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha East Africa
Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Fukayosi wilayani
Bagamoyo,mkoani Bagamoyo,wakati alipotembelea kiwanda hicho kujionea
uzalishaji wa nguzo hizo.
Picha na Mwamvua Mwinyi
…………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KIWANDA cha kutengeneza nguzo za
umeme za zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo
Fukayosi wilayani Bagamoyo,mkoani Pwani ,kimeanza uzalishaji nguzo hizo
zinazodumu kwa zaidi ya miaka 70 hivyo kupunguza gharama za kubadili
nguzo nyingine kama ilivyo kwa nguzo zilizozoeleka za miti.
Kutokana na teknolojia hiyo ya
kisasa serikali imelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza
kutumia nguzo hizo kwenye miradi mikubwa ikiwemo ule wa Stieglers Gorge
unaotarajiwa kujengwa kwenye maporomoko ya mto Rufiji.
Waziri wa Nishati Dk .Merdard
Kalemani aliyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho wilayani
Bagamoyo kujionea uzalishaji wa nguzo hizo.
Alieleza baada ya serikali kupiga
marufuku uingizwaji wa nguzo za umeme toka nchi za nje na kuruhusu
wawekezaji kutengeneza nchini sasa umefika wakati TANESCO ianze kutumia
nguzo za zege kuanzia Desemba mwaka huu kwenye miradi mikubwa.
Dk.Kalemani alisema mara
utakapokamilika mradi wa Stieglers Gorge utaweza kuzalisha megawati
2,100 ikiwa ni uzalishaji wa megawati nyingi tangu kipindi cha mwaka
1930 uzalishaji ulipokuwa megawati 1,451 hadi sasa.
Aidha ifikapo Agosti 2018 nchi
itaweza kuzalisha megawati 240 kutoka kwenye mradi wa chanzo cha umeme
cha Kinyerezi namba mbili ambapo kuanzia Desemba mwaka huu megawati 30
zitakuwa zinaunganishwa kwenye greti ya Taifa kupitia mradi huo .
Dk.Kalemani alielezea kwamba,kadri
megawati za umeme zinavyozidi kuongezeka kwenye uzalishaji mbalimbali
wa miradi ya umeme inayojengwa itatosheleza hasa kwenye viwanda .
“Mradi huo unatarajia kutumia
nguzo kati ya 500 hadi 600 na kutokana na ukubwa wake lazima tutumie
nguzo imara ambazo zinauwezo wa kudumu kwa miaka 70 kuliko kutumia nguzo
za miti ambazo zinadumu kwa miaka mitatu”
“Utumiaji wa nguzo zinazotumia
miti madhara ni kuharibu vyanzo vya maji na mazingira hivyo kaeni na
kampuni hii mshirikiane ili mradi wa Rufiji utakapoanza kutekelezwa
zitumike nguzo za zege ambapo kilometa 36 zitatumia nguzo hizo”
“Maeneo ya mbugani huwezi kutumia
nguzo za miti ama kupitisha umeme chini ya ardhi kwani lengo langu ni
kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme,”
“Mmetekeleza agizo la serikali la
awamu ya tano kuanzisha viwanda vyetu kwa kutengeneza malighafi
zitakazotusaidia wenyewe na kuokoa fedha za kununua malighafi kutoka
nje,” Huwezi kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kutegemea malighafi toka
nje ya nchi ,” alisema Dk Kalemani.
Dk.Kalemani alisema walipozuia
nguzo zisitoke nje kulikuwa na watu 29,000 walikuwa hawajaunganishiwa
umeme lakini baada ya hapo watu 20,000 waliunganishiwa umeme .
Alibainisha kama kuna mteja
hajaunganishiwa umeme zaidi ya mwezi meneja hajafanya hivyo
atachukuliwa hatua kwani changamoto ya kuchelewesha kuunganishiwa hilo
ni tatizo la meneja husika.
Akielezea juu ya kiwanda hicho
mmiliki -Otieno Igogo ambae anashirikiana na Wachina katika uzalishaji
wa nguzo hizo alisema kwasasa wanazalisha nguzo 50 kwa siku huku wakiwa
wameajili watu 70.
Alisema endapo zege hizo zitatumiwa itapunguza gharama za kuweka nyingine kama ilivyo kwa zile za miti.
Igogo alisema kuwa gharama za
ujenzi wa kiwanda hicho ni kiasi cha shilingi bilioni 13 ambapo
changamoto inayowakabili ni kukosa soko kwenye sekta za umma na binafsi
na kuiomba serikali kuwaunga mkono .
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa
mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ,alimshukuru
Waziri wa Nishati kwa kuendelea kufanikisha upatikanaji wa umeme hasa
ikizingatiwa mkoa huo ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi hapa nchini.
Alieleza wilaya ya Bagamoyo na
mkoa una mahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuwa na uwekezaji mkubwa
hasa kwenye sekta ya viwanda ambayo ina mahitaji makubwa ya umeme .
Mwanga alielezea mipango mbalimbali ya uzalishaji umeme itasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme.
Akishukuru kwa niaba ya wananchi
wa Bagamoyo Mbunge wa Jimbo hilo Dk Shukuru Kawambwa alisema
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo ule wa REA ni miradi
muhimu ambayo inakwenda kuondoa tatizo la umeme.
Dk Kawambwa alimpongeza Rais wa
awamu ya tano Dk John Magufuli kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji wa
umeme ambapo kwa miaka mingi kumekuwa na upungufu wa umeme na baadhi ya
maeneo kutokuwa na huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment