Pages

Thursday, May 25, 2017

WATANO MBARONI MREMBO KUCHOMWA MOTO ARUSHA

Watu watano wanashikiliwa na Polisi mkoani Arusha kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili waliofariki juzi kwa kuunguzwa moto wakidaiwa kuwa katika mapenzi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana wakati akizungumza na vyombo vya habari, licha ya kukataa kuwataja wanaoshikiliwa kwa madai kwamba uchunguzi bado unaendelea.

"Tunawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya wapendanao kwa kuchomwa moto," alisema.

Aliwataja waliouawa kuwa ni Denis Fasal, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 na Maureen Urio (32), wote wakazi wa jijini Arusha.

Marehemu hao walikutwa wamekufa kwa kuchomwa moto wakiwa katika chumba cha Maureen katika nyumba moja iliyopo mtaa wa Ilkiurei, katika kata ya Kirenyi, wilayani Arumeru, huku wakiwa wamefungwa kamba miguuni na mikononi na wamelala kwenye godoro lililoungua moto.

Kamanda Mkumbo alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda Mkumbo alitumia nafasi hiyo kuwashauri watu walio katika uhusiano kutojichukulia hatua pale wanapokosana na wenza wao.

Alisema kama kuna watu waliotishiwa na wapenzi wao watoe taarifa kwa polisi ili wawachukulie hatua mara moja hususani wanawake wanaokabiliwa na adha kama hiyo.
Chanzo: Nipashe

No comments: