Pages

Tuesday, January 10, 2017

KORTI YAAMURU WASHTAKIWA WA MAUAJI YA DADA WA BILIONEA MSUYA WAKATIBIWE


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru washtakiwa wa kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, wakatibiwe baada ya kukubaliana na madai yao kuwa walipigwa wakiwa mahabusu katika kituo cha Polisi.

Washtakiwa hao Miriam Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus Muyela (40), wanadaiwa kumuua Aneth, ambaye ni dada wa bilionea Erasto Msuya kwa kumchinja akiwa nyumbani kwake, Kibada Kigamboni mei 25, 2016.

Mariam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni mjane wa bilionea Msuya, aliyekuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite. Bilionea Msuya pia aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 2015 eneo la Mijohoroni, kando mwa barabara ya Arusha – Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Uamuzi wa Mahakama kwa washtakiwa kwenda kutibiwa unatokana na malalamiko yao waliyoyatoa kupitia kwa Wakili Peter Kibatala kuwa walipokuwa mahabusu, waliteswa kwa kupigwa na kulazimishwa kukubali kutenda kosa hilo katika maelezo yao.

Mbali na madai ya washtakiwa hao kuteswa na kuomba Mahakama ifanye uchunguzi na iagize watibiwe, pia Wakili Kibatala alidai hati ya madai ina kasoro za kisheria.

Mahakama ya Kisutu katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa ilikubaliana na madai ya washtakiwa hao.

No comments: