Pages

Friday, August 26, 2016

WALIOTIMULIWA UDOM KUSOMEA UALIMU WA SHULE ZA MSINGI


DAR ES SALAAM.  Wanafunzi 269 kati ya 290 waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mapema mwaka huu na ambao waliomba kuendelea na masomo ya ualimu, sasa watapelekwa kusomea ualimu wa shule za msingi na watatakiwa kujilipia ada kulingana na viwango vilivyowekwa na serikali.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo kuwa serikali imeamua kuwapeleka kwenye vyuo vyake, wanafunzi hao 269 ambao awali serikali iliwataka waombe mafunzo watakayoona yanawafaa kulingana na ufaulu wao, lakini baada ya kutafakari kwa kina na kupokea maombi kutoka kwao imeridhia kuwapeleka huko vyuoni.
 
Mwezi uliopita, serikali iliwarudisha wanafunzi 382 kuendelea na kozi hiyo ya masomo ya Sayansi na Hisabati baada ya kuthibitisha kuwa walikuwa na sifa.

Siku hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alisema wanafunzi wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu maalumu wa Stashahada ya Ualimu wa Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu, wangehamishiwa vyuo vya ualimu na wengine 1,337 wa mwaka wa pili wangehamishiwa vyuo vya Korogwe na Kasulu ili kumalizia masomo yao.

Prof. Ndalichako alisema wanafunzi wengine 29 wa mwaka wa pili ambao wana cheti cha daraja A la Ualimu, wangehamishiwa Chuo cha Ualimu Kasulu ili wamalize masomo yao ila kwa gharama zao wenyewe, huku wengine 1,181 wakitakiwa waombe nafasi kwenye vyuo vingine kwa masomo ambayo wana sifa stahili.
Chanzo: Mwananchi

No comments: