Pages

Thursday, April 28, 2016

POLISI WAUA MAJAMBAZI WATATU MBEYA

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Butusyo
MBEYA.  Watu watatu kati ya watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa katika tukio la kurushiana risasi na Polisi ambao walikuwa wakijaribu kuzuia uporaji kwenye duka la jumla lililopo Matundasi wilayani Chunya.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Butusyo Mwambelo amesema tukio hili lilitokea jana saa 2:00 usiku katika kijiji cha Matundasi na inadaiwa majambazi hao walitumia pikipiki mbili, moja ikibeba watu watatu na nyingine wawili.

Amesema kuwa Polisi walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema na kujipanga kukabiliana nao na kwamba walipofika katika duka la jumla la bia ndipo Polisi walipowaona na kuanza kupambana nao.

"Katika mapambano hayo jambazi mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Baraka, ambaye ni fundi bomba na mkazi wa Makongorosi aliyekuwa na silaha aina ya SMG iliyokuwa na risasi 26, aliuawa baada ya kupigwa risasi tumboni na mguuni,"alisema.

Butusyo alisema majambazi wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea kijiji cha Matondo na ndipo askari polisi walipoendesha msako mkali katika kijiji hicho na baada ya kuwaona Polisi waliwasha pikipiki zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi ovyo.

"Ndipo Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwauwa majambazi wengine wawili na kukamata pikipiki moja aina ya Sanlg iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao,"alisema.
Chanzo:  Mwananchi

No comments: