Pages

Friday, January 3, 2014

UYUI WAOMBA RAIS KIKWETE AINGILIE KATI BEI YA UMEME


WANANCHI wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora wameomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kupanda kwa bei ya umeme na gesi.

Ombi hilo lilitolewa jana kwenye mdahalo, uliohusu mabadiliko ya tabia nchi pamoja na madhara.  Mdahalo huo uliandaliwa na taasisi ya Ucoden kwa ufadhili wa taasisi ya Foundation for Civil Society ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika mdahalo katika kijiji cha Kigwa wilayani Uyui, Kamugisha Ngaiza alisema kupanda kwa umeme, kutasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, kwani asilimia kubwa ya watu nchini hawana uwezo kabisa wa kumudu bei hiyo mpya.

Alisema wananchi waishio vijijini ndio vinara wa kuharibu mazingira kutokana na kukata miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kupikia na shughuli za kilimo.

Pia, wananchi hao walipendekeza gesi iuzwe kwa kuzingatia hali halisi ya maisha ya mtanzania ili kila mtu aweze kuimudu.

Walisema gesi ikiuzwa bei nzuri kwa wananchi, hasa wa vijijini, itasaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira, ambao unaweza kuleta ukame na kusababisha mvua kutonyesha.

Mratibu wa uconden, Christopher Nyamwanji alihimiza matumizi ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia, kwani ni njia mojawapo ya kukabili uharibifu wa mazingira.

No comments: