TUME ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) imesema mkoa wa Njombe ndio unaoongoza kwa kuwa na maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1.
Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya nne kwa asilimia 9 ukifuatiwa na Ruvuma (7.2), Shinyanga (7.4), Dar es Salaam (6.9), Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9), Tabora (5.1), Kagera (4.8) na Geita (4.7).
Msemaji wa TACAIDS, Gloria Mziray amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mikoa mingine na viwango vyake ni Mara (4.5), Mwanza (4.2), Mtwara (4.1), Kilimanjaro (3.8), Kigoma (3.4), Simiyu (3.6), Morogoro (3.8), Singida (3.3), Dodoma (2.9), Manyara (1.5), Lindi (2.9), Tanga (2.4), Unguja (1.9) na Pemba (0.3).
Amesema takwimu hizo zinatokana na utafiti uliofanyika mwaka juzi hadi mwaka jana. Kutokana na matokeo hayo, amesema maambukizi ya UKIMWI yamepungua kwa kasi ndogo.
Amesema watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu virusi vya UKIMWI na UKIMWI wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia.
Kuhusu tohara kwa wanaume, endapo inapunguza maambukizi ya Ukimwi alisema kuwa inapunguza kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo.
Source: Michuzi blog
No comments:
Post a Comment