![]() |
John Tendwa, Msajili wa Vyama mstaafu. |
BAADA ya misukosuko ya kisiasa ya hapa na pale na hasa kulalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini, hatimaye Msajili wa Vyama hivyo, John Tendwa amestaafu utumishi wa umma. Nafasi yake imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Jaji Mutungi anakuwa Msajili wa Vyama vya Siasa wa tatu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, nafasi hiyo ilipochukuliwa kwa mara ya kwanza na George Liundi.
Kutokana na uteuzi huo, baadhi ya wadau wa siasa wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa nchini wamempongeza Rais Kikwete kwa kumteua Jaji Mutungi na kumtaka aendeleze mema ya Tendwa na kusimamia sheria ipasavyo, bila kupendelea.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Dar es Salaam ilieleza kuwa, uteuzi huo ulianza Agosti 2. Kwa mujibu wa taarifa, kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.
Source: habarileo
No comments:
Post a Comment