Pages

Friday, April 12, 2013

WAANDISHI WAWILI NA AFISA UHAMIAJI WAFARIKI DUNIA AJALINI


Marehemu Hussein Semdoe akiwa kazini. Picha hii ilipigwa mwishoni mwa wiki Kwamsisi wilayani Handeni mkoani Tanga


Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu akiwa kwenye kazi za kijamii Kwedikabu, Kwamsisi mwishoni mwa mwaka jana.  Mwenye Kamera ni marehemu Semdoe.
(picha na story kutoka fatherkidevu blog)

WATU watatu, wakiwamo waandishi wa habari wawili, Hussein Semdoe wa gazeti la Mwananchi na Hamis Bwanga wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni, Mariam Hassan wamefariki papo hapo katika ajali iliyotokea leo Misima, wilayani Handeni mkoani Tanga.

Watu hao walikuwa wakitoka Misima katika shughuli za kikazi na kusababisha vifo hivyo vilivyopokelewa kwa uchungu mkubwa na Watanzania wote, wakiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu.

Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wilayani humo, Simon Mdaki, amesema kuwa ajali hiyo imetokea baada ya gari walilokuwa wanasafiria kupasuka tairi la mbele, hivyo dereva kushindwa kulimudu na gari hilo kupinduka.

Alisema gari hilo lililopata ajali lilikuwa nyuma ya gari ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Rweyemamu ambaye alikuwa ameongozana na marehemu hao katika shughuli za kikazi Misima, Handeni.

"Mkuu wa Wilaya yeye hajaumia kwasababu gari lake lilikuwa la mbele, ingawa gari hilo lililopata ajali lilikuwa kwenye msafara wake.  Tumeguswa sana na vifo hivi vilivyotokea katika wilaya yetu,” alisema Mdaki.

Vifo vya waandishi hao ambao wana mchango mkubwa wilayani humo vitakuwa ni pigo kwa Watanzania wote, wakiwamo wananchi wa Handeni ambao kwa hakika mikono ya waandishi hao ilitumika vyema kuhabarisha umma kwenye vyombo vyao. 

MUNGU AZILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO ZA MAREHEMU.

No comments: