Pages

Tuesday, April 9, 2013

UHURU KENYATA KUAPISHWA LEO, RAIS KIKWETE KUHUDHURIA SHEREHE HIZO


Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya.

Wananchi wa Kenya leo wanasuburi kwa hamu sherehe ya kihistoria ya kumuapisha Rais mteule wa taifa hilo Uhuru Muigai Kenyatta ambazo zitafanyika katika viwanja vya Kasarani Nchini humo.

Kuna hali ya msisimko na matarajio ya wengi, hasa utendaji kazi katika serikali mpya ya Kenya.

Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi dhidi ya wagombea wengine saba(7) waliosimama kuwania kiti cha urais.

Kutokana na ushindani uliokuwepo hata katika kura ya maoni, ilidhihirisha kuwa kinyang’anyiro kilikuwa kikali kwa wagombea wawili, Raila Odinga wa chama cha ODM, na Uhuru Kenyatta wa chama cha TNA.

Uhuru Kenyatta alishinda  kwa zaidi ya kura 700,000 na baada ya Mahakama ya juu nchini Kenya kuamua kesi iliyowasilishwa na bwana Odinga ya kupinga matokeo ya ushindi wa Rais katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwanzoni mwa mwezi Machi, Bwana Odinga alikubali uamuzi wa Mahakama.

Hatua hiyo iliondoa wasiwasi kwa watu waliohofia kuwa huenda Kenya ikakumbwa tena na mgogoro wa kisiasa na ghasia, kama zile zilizotokea mwaka  2008.
 
Wakati huo huo taarifa kutoka serikalini  inasema kuwa marais  13 walioalikwa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wanne wa Jamhuri ya Kenya, bwana Uhuru Kenyatta wamethibitisha kuhudhuria.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amepangiwa kutoa hotuba kwa niaba ya marais wengine watakaohudhuria. 

Sherehe hiyo ya kitaifa pia itaashiria siku ya mwisho kwa Rais Mwai Kibaki kuwa ofisini kama Rais wa Kenya.

Rais Jakaya Kikwete akipokea shada la maua mara baada ya kuwasili mjini Nairobi.

Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakipokea mashada ya maua mara  baada ya kuwasili  uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata jijini Nairobi tayari kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo Mhe Uhuru Kenyata; sherehe zitakazofanyika katika viwanja vya Kasarani jijini Nairobi.


No comments: