YANGA, KOCHA VPL WAPIGWA FAINI
KLABU
ya Yanga na Kocha Msaidizi wa timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa
faini ya sh. 500,000 kila mmoja kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea nchini.
Adhabu
hizo zimetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) iliyokutana Jumapili (Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia
ripoti za waamuzi na makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171.
Yanga
imepigwa faini hiyo baada ya kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya
Kagera Sugar iliyochezwa Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa
faini ya sh. 100,000 kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi
(pre match meeting) dhidi ya African Lyon
iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
Naye
Kocha Bilali amepigwa faini hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa
kumshambulia kwa maneno kocha wa timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi
amtoe kwenye benchi la wachezaji. Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na
Tanzania Prisons iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.
African
Lyon na Simba zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa kuchezesha
timu zao za U20 kwenye mechi za utangulizi wakati zilipocheza na Oljoro JKT na
Coastal Union , Machi mwaka huu kwenye viwanja
vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.
Suala
la Meneja wa Coastal Union , Akida Manchai
kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti wake Steven
Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na Coastal Union iliyochezwa
Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya Nidhamu kwa
ajili ya hatua za kinidhamu.
Adhabu
zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom.
POLISI KUJIULIZA KWA RUVU SHOOTING VPL
Polisi
Morogoro inapambana na Ruvu Shooting katika moja kati ya mechi tatu za Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa kesho (Aprili 10 mwaka huu). Matokeo ya mechi
hiyo yanatarajia kutoa mwanga kama Polisi
inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Timu
hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mechi hiyo
itakayochezeshwa na Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga akisaidiwa na Godfrey Kihwili
na Ephrony Ndissa wa Arusha.
Polisi Morogoro inayonolewa na Adolf Rishard
inakamata nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza mechi tatu dhidi
ya Simba, Kagera Sugar na Coastal Union.
Mechi
nyingine za kesho ni kati ya Tanzania
Prisons iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo Shooting. Mwamuzi
Hashim Abdallah wa Dar es Salaam
ndiye atakayechezesha mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya. Mgambo ina pointi 24 na iko katika nafasi ya tisa.
Mwamuzi
Said Ndege wa Dar es Salaam
atachezesha mechi kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans itakayofanyika
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans ya Kocha John
Tegete ina pointi 21 ikiwa nafasi ya 11 wakati Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano
na pointi zake 32.
Ligi
hiyo itaendelea keshokutwa (Aprili 11 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Azam na
African Lyon itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.
KAMATI YAZIPONGEZA ASHANTI , MBEYA CITY ,
RHINO
Kamati
ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezipongeza timu za Ashanti United ya Dar es
Salaam , Mbeya
City ya Mbeya na Rhino
Rangers ya Tabora kwa kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2013/20114).
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Wallace Karia amezitaka timu hizo kufanya maandalizi ya kutosha
ili ziweze kushindana katika VPL ikiwemo kutimiza masharti ya kuwa klabu za
Ligi Kuu.
Moja
ya masharti ya klabu zenye hadhi ya Ligi Kuu ni kuwa na timu ya pili (U20)
ambayo itakuwa na inacheza mechi za utangulizi kwenye uwanja wa nyumbani kila
timu ya wakubwa inapocheza.
Mbali
ya kuthibitisha timu hizo tatu kupanda daraja, pia Kamati ya Ligi imethibitisha
rasmi timu tatu zilizoshuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa katika mkoa husika. Timu
zilizoshuka kutoka Daraja la Kwanza (FDL) ni
Small Kids ya Rukwa kutoka kundi A.
Kundi
B timu iliyoshuka ni Moro United ya Dar es Salaam wakati Morani FC ya Manyara
yenyewe imeporomoka kutoka kundi C.
No comments:
Post a Comment