Pages

Thursday, April 4, 2013

JAJI MSTAAFU ERNEST MWIPOPO AFARIKI DUNIA


Marehemu Jaji Ernest Mwipopo, enzi za uhai wake.

Jaji mstaafu Ernest Mwipopo (63) ambaye pia ni mjumbe wa Tume ya kurekebisha Katiba, amefariki dunia jana mchana baada ya kupata ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Mkata, Kata ya Doma, wilaya ya Mvomero, katika barabara kuu ya Iringa - Morogoro.
Ajali hiyo imetokea wakati Jaji akitoka mkoani Iringa kwenye mapumziko ya Pasaka akirejea nyumbani kwake Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, marehemu alifariki baada ya gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba T691 AUL kupasuka tairi la mbele, kuacha njia na kupinduka mara tatu.
Kamanda Shilogile amesema kuwa gari hiyo ilikuwa na abiria wengine wanne (4) ambao wote wamejeruhiwa na wamelazwa katika hospitali ya mkoa ya Morogoro.
Hata hivyo alisema, mwili wa Jaji huyo umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ukisubiri taratibu nyingine kutoka mamkala zinazohusika pamoja na ndugu wa marehemu.

Mbali na hayo amesema kwamba uchunguzi zaidi kuhusiana na ajali hiyo unaendelea kufanywa na Polisi .
MUNGU AILAZE PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU
JAJI MSTAAFU ERNEST MWIPOPO.

No comments: