Pages

Monday, April 11, 2022

WAZIRI NAPE AANZA ZIARA KUKAGUA MWENENDO WA OPERESHENI ANWANI ZA MAKAZI


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 11,2022 katika katika uwanja wa ndege jijini Dodoma kabla ya kuanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kufanya uhamasishaji wa uwekaji anuani za makazi.


WAZIRI wa  Habari  Mawasiliano  na Teknolojia ya  Habari,Nape Nnauye ameanza ziara ya  kuzunguka Nchi nzima kwa njia ya usafiri wa Helcopta  kuhamasisha zoezi la uwekaji wa anwani za makazi ambapo amedai kwa sasa zoezi hilo  limefikia  asilimia 68 huku akiitaja Mikoa ya Dar es salaam na Tanga kuwa bado haijafanya vizuri.

Akizungumza leo,Aprili 11,2022 akiwa uwanja wa Ndege wa Dodoma tayari kwa safari  ya kuanza zoezi hilo kwa leo katika Mikoa ya Tanga,Kilimanjaro na Arusha,Waziri Nape amesema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alizindua operation ya kuhakikisha kila mtanzania ana anwani ya makazi katika eneo analoishi na kufanyia kazi.

“Tathmini yetu inaonesha tumefikia asilimia takribani 68 lakini bado kuna baadhi ya maeneo kuna changamoto kuna Mikoa bado haifanyi vizuri sana ikiwemo Mkoa wa Dar es salaam na Tanga na kuna baadhi ya Mikoa inafanya vizuri kama Lindi na mingine ambayo ipo katikati.

“Katika mazingira hayo tunatakiwa kukabidhi ufunguo tarehe 22 mwezi wa tano mwaka huu sasa kwa muda uliobaki tumekubaliana tuongeze nguvu katika hamasa pamoja na uwekaji wa alama.

“Sasa asubuhi ya leo naondoka mimi na Katibu Mkuu na watendaji tunaenda Mikoa mitatu kwa leo,tutakuwa  Tanga na  mchana Kilimanjaro na jioni Arusha halafu kesho tutapumzika na tutaendelea kushokutwa hii ni operation ya Mikoa yote kwa siku tutafanya  ziara zaidi ya mikoa mitatu hadi minne ndio maana tunatumia Helcopta tunataka kuona maeneo hayo vizuri,”amesema.

Waziri Nape ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Nchi ikiwa ni pamoja na kuhamasishana ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.

“Nitoe wito kwa watanzania jambo hili ni la kwetu na mfumo huu utatusaidia sana sina shaka manufaa yameeleweka, nawaomba kila mtanzania aone aibu kukaa mahali ambako nyumba yake haina anwani.

“Lakini pia si vibaya kumsukuma jirani yako ambaye hana anwani ya makazi.Ni matumaini yangu tukishirkiana kwa pamoja tutaiweka katika Nchi za kistaarabu.Wito wangu asubuhi ya leo tumuunge mkono mama Samia,”amesema.

 Katika  ziara hiyo Waziri Nape ameambatana na Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na baadhi ya wataalamu ambapo wanatumia usafiri wa helkopta ili kuifikia mikoa zaidi ya mitatu kwa siku, kwa kuwa zoezi hilo ni operesheni maalumu na Wizara imejipanga kwenda kuona mwenendo wa utekelezaji na kuongeza nguvu maeneo yenye Changamoto.

No comments: