Pages

Tuesday, April 12, 2022

RIPOTI YA CAG INAONYESHA MAKUSANYO YA SH.BILIONI 17 HAYAJAPELEKWA BENKI


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 12,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu  uwasilishaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni,2021.  

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 12,2022 jijini Dodoma mara baada ya kutoa taarifa kuhusu  uwasilishaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni,2021.  

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) Mhe.Grace Tendega,akizungumza mara baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere,kutoa taarifa kuhusu  uwasilishaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni,2021 leo April 12,2022 jijini Dodoma.

SEHEMU ya washiriki wakifatilia hotuba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere,(hayupo pichani) leo April 12,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu  uwasilishaji wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni,2021. 

……………………………………………        

Na Alex Sonna-DODOMA

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia June 30 2021 inaonesha  wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 17.

Pia,Mashirika 14 ya kibiashara yanajiendesha kwa hasara ikiwemo    Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na  Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 12,2022 Jijini hapa mara baada ya asubuhi kuiwasilisha ripoti hiyo bungeni,Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 17.

MASHIRIKA 14 YANAJIENDESHA KIHASARA

Kichere amesema  kwa miaka miwili 2019-2020 na 2020-2021 mashirika 14 ya kibiashara yalipata  hasara mfululizo.

“Hali hiyo ilisababishwa na hasara kwenye uwekezaji uliofanywa,ufanisi duni wa mashirika husika na udhibiti hafifu wa mapato na matumizi,”amesema.

Amesema kampuni ya ATCL kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya sh. Milioni 36,499.20 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara y ash.milioni 60.

C.A.G amesema Kampuni ya Biotech Production kwa mwaka 2020-2021 imepata hasara ya sh. Milioni 14,779.56 na mwaka 2019-2020 ilipata hasara ya sh.milioni 15,073.79.

Ameyataja Makampuni mengine yaliyojiendesha kwa hasara ni Kampuni ya Mkulazi,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Kiwanda cha Kimataifa cha bidhaa za ngozi Kilimanjaro,(KILC),Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC),Shirika la uuzaji bidhaa Tanzania (EPZA).

Pia,Kampuni ya Kuzalisha nguo za umeme za zege Tanzania (TCPM),Shirika la Posta Tanzania (TPC),Kampuni ya Nyumba za watumishi (Watumishi Housing),Kampuni ya T-PESA kampuni tanzu ya TTCL,Kampuni ya uwekezaji ya PPF,DCC,Kampuni ya uchapishaji ya Chuo Kikuu Dar es salaam (DUP) na Kampuni ya Umeme ya Kikuletwa.

C.A.G amesema hati za ukaguzi zinaonesha katika Mamalaka za Serikali za Mitaa kati ya hati 185 zinazoridhisha ni  178 zenye shaka sita,hati mbaya ni moja.

HATI MBAYA NA ZENYE MASHAKA

Amesema Mashirika ya umma 195 yenye hati zinazoridhisha ni 185 yenye hati zenye  shaka ni  nane hati mbaya hakuna na yaliyoshindwa  kutoa maoni ni  mawili.

Kwenye Serikali Kuu amesema  kati ya hati 308 hati zinazoridhisha ni 305 zenye shaka mbili,hati mbaya moja na hakuna ambayo imeshindwa kutoa maoni.

HALMASHAURI

Amesema Halmashauri zilizopata hati zenye mashaka ni ya Wilaya ya Kisarawe,Longido,Mlele,Musoma,Halmashauri ya Sengerema na Bunda.

Kwa upande wa Mashirika ya Umma ameyataja yenye hati zenye mashaka ni pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita,Taasisi ya Mifupa Muhimbili,Mamlaka ya Bandari Tanzania,Kampuni ya Magazeti ya Tanzania,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Amesema kwa upande wa Serikali kuu,Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) imepata hati yenye mashaka pamoja na Hesabu Jumuifu za Taifa huku Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) likipata hati mbaya.

Aidha,C.A.G amesema wakusanya mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 147 hawakuwasilisha benki makusanyo yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 17.

Pia,Mawakala wa kukusanya mapato katika Mamkala za Serikali za Mitaa 12 hawakupeleka benki makusanyo ya shilingi bilioni 3.31 kinyume na mikataba yao.

“Ninapendekeza kwamba Tamisemi iongeze usimamizi wa mapato na kuhakikisha makusanyo yanapelekwa benki bila kuchelewa,”amesema.

Vilevile,amesema Mamlaka ya Serikali za Mitaa 24 zilitumia sh.milioni 664 katika matumizi yasiyo na manufaa kama vile malipo kwa riba na adhabu za kuchelewesha malipo na posho kwa watumishi wasiostahili.

Aidha,Mamkala za Serikali za Mitaa 61 ziliagiza na kulipa sh bilioni 8.44 kwa ajili ya bidhaa ambazo hazikuwasilishwa  na wazabuni kwa muda wa hadi kufikia miezi 24.

 

 

No comments: