Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akiangalia
moja ya kazi zinazofanywa na Vyuo vikuu nchini alipotembelea mabanda ya
maonesho wakati wa kufunga Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na
Teknolojia yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es
Salaam.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (Mb) amesema
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Sekta ya Elimu ya Juu imepata
mafaniko makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la udahili na
uimarishaji mifumo ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Naibu
Waziri Kipanga amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga
Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema
idadi ya wanafunzi wa Shahada ya kwanza kwenye vyuo vya Elimu ya juu
imeongezeka kutoka 65,064 mwaka 2015/16 hadi 87,934 mwaka 2020/21 huku
wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wakiongezeka kutoka wanafunzi
125,126 mwaka 2015 hadi 132,392 mwaka 2020.
Ameongeza
kuwa katika kuhakikisha Vyuo Vikuu vinatoa elimu bora ya kiushindani
ndani na nje ya Nchi, mifumo ya uthibiti ubora imeendelea kuimarishwa
ikiwemo mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji na mifumo ya uhakiki na
utambuzi wa sifa za kitaaluma za wahitimu wa Elimu ya Juu zilizotolewa
na vyuo vya nje ya nchi.
“Pamoja
na mafaniko hayo makubwa pia tumeboresha miundombinu ya kufundishia na
kujifunzia katika ngazi zote za elimu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa
madarasa, kumbi za mihadhara, maabara, maktaba, hosteli na ununuzi wa
vifaa vya utafiti, pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia,”
amesema Mhe. Kipanga.
Aidha
Naibu Waziri Kipanga ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa vyuo vikuu na
taasisi nyingine za elimu ya juu kuendelea kufanya mapitio ya mitaala
ili iendane na mahitaji ya soko la ajira kwa kuweka msisitizo katika
masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), pamoja na
utoaji wa mafunzo kwa vitendo.
Pia
amendelea kuvitaka vyuo hivyo kuweka mikakati ya kuzalisha wataalamu
wa kutosha hususani katika sekta adimu na zenye tija kwa maendeleo ya
nchi yetu ili kufikia lengo la kitaifa la kuwa na wahitimu 98,000 kwa
mwaka ifikapo mwaka 2025/26.
Kwa
upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof.
Charles Kihampa amesema maonesho ya mwaka 2021 yamekuwa na mafanikio
makubwa kwa kupata washiriki wengi na kwamba zaidi ya waombaji elfu 52
wa Shahada ya kwanza wametuma maombi katika vyuo mbalimbali na kati ya
maombi hayo mengine yamefanyika moja kwa moja kupitia maonesho.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wanafunzi waliohitimu kidato cha sita ambao
wangependa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, wameipongeza Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania kwa kufanya maonesho hayo kwa kuwa wamepata fursa ya
kukutana na vyuo vyote katika eneo mmoja na kufanyiwa udahili bila
gharama yoyote.
Maonesho
ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoanza *Julai 26* na
kuhitimishwa Julai 31 yalikuwa na kauli mbiu isemayo “Kuendelea Kukuza
na Kudumisha Uchumi wa Kati kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na
Teknolojia”.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akizungumza
wakati wa kufunga maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Waombaji
wa vyuo vya Elimu ya Juu wakifanyiwa udahili wa moja kwa moja kutoka
kwenye mabanda ya maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Mmoja
wa washiriki wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
akipokea cheti cha utambuzi wa kushiriki maonesho hayo kwa mwaka 2021.
Baadhi
ya washiriki wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Mhe. Omary Kipanga (hayupo pichani) wakati wa kufunga maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment