
Na ABRAHAM GWANDU, ARUSHA
MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, amesema vitendo vya
polisi kuwakamata waandishi wa habari wanapokuwa katika majukumu yao ya
taaluma siyo msimamo wa jeshi hilo bali ni la bahati mbaya.
Alisema waandishi na vyombo vya habari ni wadau muhimu wa jeshi hilo lazima washirikiane nao.
IGP Mangu alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada
ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi
wa nchi za Kusini mwa Afrika (Sarpcco) unaoendelea Arusha.
“Askari anapokuwa katika eneo la tukio anakuwa na tabia fulani ambayo
kila mmoja wetu anayo kulazimisha mambo, ninyi ni wadau wetu lazima
tufanye kazi pamoja hatuna ugomvi wowote na waandishi.
“Yanapotokea matukio ya aina hiyo ya kukamatwa au
kusumbuliwa tujulishane kwa sababu askari wadogo wakati mwingine hufanya
vitu ambavyo siyo msimamo wetu sisi viongozi wao,” alisema IGP Mangu.
Mangu pia alizungumzia matukio ya mauaji yanayoendelea wilayani Kibiti
Mkoa wa Pwani akisema ni uhalifu kama ulivyo mwingine wa kawaida na
usitafsiriwe vinginevyo kwa sababu tayari umeanza kudhibitiwa.
Wakati IGP Mangu akisema hivyo, vyombo vya usalama vinawashikilia watu
zaidi ya 60 katika mahabusu ya gereza la Kisongo kwa tuhuma za kuhusika
na ugaidi ikiwamo kurusha bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi Olasiti.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Hamadi Massauni alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na
nchi wanachama wa Sadc kuhakikisha uhalifu wa kuvuka mipaka
unadhibitiwa.
Naye Katibu Mtendaji wa Sadc, Stegomena Tax, aliwahakikishia wakuu hao
wa polisi kuwa Jumuiya anayoingoza itaendelea kutoa misaada na
ushirikiano kila unapohitajika kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment