Pages

Friday, March 31, 2017

MAKONDA AKWEPA KUZUNGUMZIA SHAURI LAKE

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema taarifa yoyote kuhusu yeye kuhojiwa na Bunge ipo katika mamlaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambayo ndiyo iliyomhoji.

Makonda aliyasema hayo akijibu swali la mwandishi wa habari wa gazeti hili kuhusu mkutano wake huo wa mahojiano na kamati hiyo ya Bunge.

“Ni kweli nimehojiwa ila yale ya kule (katika kamati) yanabaki kule kule, siwezi kuyaleta huku. Nadhani Mwenyekiti wa kamati (George Mkuchika) alizungumza jana kuhusu hilo, nadhani kama mna maswali zaidi, aulizwe yeye,” alisema Makonda.

Juzi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilimhoji Makonda kwa saa tatu kuhusu tuhuma za kuingilia madaraka ya mhimili huo wa dola.

Baada ya mahojiano hayo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mkuchika alisema kamati imemaliza kazi na taarifa yake itaiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Makonda alifika mjini hapa juzi kuitikia mwito wa kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa Februari 8, mwaka huu katika kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge kwamba Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam ahojiwe na Bunge.

Katika kikao hicho, Bunge liliazimia kwamba Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti waitwe mbele ya Kamati hiyo ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia Bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.

No comments: