Pages

Saturday, July 18, 2015

SAFARI YA WEMA SEPETU IMEIVA, UBUNGE VITI MAALUM MKOA WA SINGIDA

DSC00396
Picha ya chini na juu ni Wema Sepetu (kushoto) akipokea fomu za kuwania ubunge viti maalum mkoa wa Singida kutoka kwa Katibu wa UWT wilaya ya Ikungi, Yagi Kiaratu.

DSC00401

DSC00393
Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu akilipa ada ya fomu ya kuwania ubunge viti maalum mkoa wa Singida (17/7/2015).  Kulia ni Katibu UWT wilaya ya Ikungi mkoani Singida.


DSC00403
Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu akitoka ndani ya ofisi ya CCM wilaya ya Ikungi baada ya kukabidhiwa fomu za kuwania ubunge viti maalum mkoa wa Singida.  Nyuma ni mama yake, Bibi Mariamu Sepetu.(Picha na Nathaniel Limu).

MSANII wa filamu maarufu nchini ambaye pia ni Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Isaac Sepetu, jana amechukua fomu ya kuomba kugombea nafasi ya viti maalimu CCM mkoa wa Singida na kuahidi kwamba lengo lake ni kuja kushirikiana na wanawake na wakazi kwa ujumla kuuletea maendeleo zaidi mkoa huo.

Wema ameahidi kutumia nguvu zake zote na uzoefu wake katika kutumikia jamii, kusaidiana na wanawake katika kujiletea maendeleo yakiwemo ya uchumi.

Alisema kwa muda mrefu amekuwa akiisaidia jamii ya jijini Dar-es-Salaam na sasa ameamua kwa dhati kuelekeza nguvu zake katika kuitumikia jamii ya nyumbani kwao mkoa wa Singida.

“Pia natarajia kukaa chini na vijana wa mkoa wangu wa Singida,ili kwanza nijue changamoto zinazowakabili halafu kwa pamoja tuweke mipango na mikakati ya namna ya kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto hizo,” alisema.

Wema pia amesema kuwa ataelekeza nguvu zake kwa wanawake, asikie vilio vyao ili aweze kupata mwelekeo wa namna ya kuwasaidia waweze kujiendeleza kwa manufaa ya familia zao, mkoa na taifa kwa ujumla.

Kuhusu sekta ya usanii alisema endapo CCM kitampitisha na kufanikiwa kuwa Mbunge wa viti maalum, atatumia fursa ya kuwa kiongozi mwenye uwezo wa kuwasaidia wasanii mbalimbali pamoja na mambo mengine, wasiibiwe kazi zao.

“Kwa kweli niwahakikishie wasanii wenzangu kuwa nikifanikiwa kuwa kiongozi, nitahakikisha kazi zao hazitaibiwa tena na pia kuwepo kwa mazingira rafiki yatakayo wasaidia kufanya kazi zao bila vikwazo vyovyote,”alisema Wema.
Chanzo: Dewji Blog

No comments: