Pages

Sunday, July 12, 2015

MWANAFUNZI AGONGWA, WAKAZI WACHOMA MOTO KITUO CHA POLISI

Askari wakimdhibiti kijana aliyetuhumiwa kuhusika na tukio la kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju ‘A’ kilichopo nje kidogo ya Jiji la DSM. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Wakazi wa Bunju ‘A’, wamechoma kituo cha polisi cha eneo hilo kwa kile kilichodaiwa kushindwa kuelewana na askari baada ya mwanafunzi wa darasa la nne kugongwa na gari na kufariki dunia.

Tukio hilo lilitokea jana saa tatu asubuhi gari aina ya Toyota Coaster lilipomgonga mwanafunzi huyo, Thabitha Omari (11) aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Bunju ‘A’.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura alifika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya wakazi hao waliomweleza kuwa wanataka matuta yawekwe barabarani karibu na eneo la shule ili kupunguza mwendokasi wa madereva wa magari.

Walimweleza kuwa eneo hilo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara.
Hata hivyo, wakati Kamanda Wambura akifanya jitihada za kuzungumza na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Kinondoni, ili waje waweke matuta yaliyokuwa yakidaiwa, ghafla kundi la watu lilivamia kituo cha Polisi na kukichoma moto.

Akizungumzia kitendo hicho, Kamanda Wambura alisema: “Hatua kali za kisheria zitachukuliwa na tutahakikisha wahusika wanakamatwa kwakuwa wamesababisha hasara ya mali na nyaraka zilizokuwamo ndani na nje ya kituo.”
Alisema kituo hicho kimejengwa kwa nguvu ya umma kutokana na mahitaji ya wengi, hivyo vurugu za watu wachache kujichukulia sheria mkononi inawakosesha haki ya ulinzi na usalama wengi.

Awali, baada ya mwanafunzi huyo kugongwa, wanafunzi walifunga barabara ya Dar es Salaam - Bagamoyo kwa muda wa saa kadhaa na kuamua kuandamana kuelekea kituo cha Polisi kabla hakijachomwa moto.

Hata hivyo, maandamano hayo yalivamiwa na kundi la watu waliochukua mwanya huo kufanya uhalifu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kihonzile, Jihadi Abdallah amelaani kitendo kilichotokea kwani hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya tukio la kugongwa kwa mwanafunzi na kuchomwa kituo moto, akisema labda kulikuwa na mambo mengine.

Mkazi wa Bunju ‘A’ Husna Shabaan ni miongoni mwa watu waliopata hasara ya kuharibiwa kwa gari lake lililokuwa limeegeshwa karibu na kituo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amewataka raia kuwa rafiki wa polisi badala ya kuwa maadui kwani wao ndiyo hulinda usalama wao na mali zao.

No comments: