Kilimo ni eneo la kipaumbele katika uchumi
wa Tanzania licha ya kuwa kilimo nchini bado kinategemea kwa kiasi
kikubwa mvua na hali ya hewa kwa ujumla .
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka ya hali ya
hewa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi zinasema mvua za
masika zimeshaanza katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua
kwa mwaka. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani
katika maeneo mengi. Hata hivyo maeneo machache yanatarajiwa kupata mvua
za wastani hadi chini ya wastani.
Hali ya unyevunyevu wa udongo inatarajiwa
kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo katika maeneo mengi.Hata hivyo,
mvua za juu ya wastani zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha hali
ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi hivyo kuathiri mazao na hata
kusababisha mafuriko na kuharibu mazao.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania, msimu wa mvua za Masika katika kipindichamiezi ya Machi hadi
Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini
Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), Pwani ya Kaskazini,
(Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-Kaskazini pamoja na
Visiwa vya Unguja na Pemba), Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera,
Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa
Kigoma.
Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa
maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya Kusini mwa ukanda huo
yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
tahadhari imetolewa kwa wakulima wote kuwa makini na mvua hizi za masika
zinazoendelea kwani zinatarajiwa kunyesha kwa wingi katika baadhi ya
maeneo kulingana na uelekeo wa upepo katika maeneo mengi ambayo
yanayopata mvua za msimu wa masika.
Mwelekeo wa mvua uliotolewa na Mamlaka ya
Hali ya Hewa hivi karibuni umezingatia zaidi kipindi cha msimu(miezi
mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria
vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi
katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa
kati na mfupi.
Wakulima wanashauriwa kuendelea na shughuli
za kawaida za kilimo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu
za kuongeza uzalishaji, kupanda mazao na miti kuzuia mmomonyoko wa
udongo pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo katika
matumizi sahihi ya ardhi na mbegu. Hata hivyo, katika maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani,upungufu wa unyevunyevu
wa udongo unaweza kujitokea hususan katika vipindi vya kukosekana kwa
mvua. Wakulima waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa
maafisa ugani katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo Sokoine(SUA) katika tafiti zao wametoa ushauri kuhusu namna
bora ya kilimo cha baadhi ya mazao kwa kuzingatia taratibu sahihi za
kilimo za mazao hayo wakati huu wa mvua za masika.
No comments:
Post a Comment