Na Tiganya Vincent_MAELEZO-Dodoma.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu imeshauri Serikali kuharakisha ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha standard gauge ili kuisaidia Bandari ya Dar es salaam
kukabiliana na ushindani kutoka bandari ya nchi jirani.
Hatua hii itasaidia kuleta
maendeleo ya haraka hapa nchini kupitia upokeaji na usafirishaji wa
mizigo mingi ya nchini na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini
Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Profesa
Norman Sigala wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti
ya Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ya mwaka ujao wa fedha.
Amesema kuwa nchi nyingine za
wanachama wa Afrika Mashariki zinaendelea kujenga reli kwa kiwango cha
standard gauge kutoka Mombasa kupitia Nairobi , Kampala hadi Kigali kwa
kasi kubwa.
Mhe. Profesa Norman alisema
kuwa ili Bandari za Tanzania ziweze kushindana na Bandari za Kenya
katika kupokea mizigo ya nchi za Uganda na Rwanda ni vema reli ya kati
ikajengwa kwa kiwango cha standard gauge ili iziunganishe nchi hizo na
reli inawezesha kusafirisha mizigo bila vikwazo.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa reli kwa kiwango hicho itasaidia kuwanufaisha mikoa 15 ya Tanzania bara.
Profesa Norman alisema kuwa ni
vema Serikali ikaharakisha ujenzi wa reli ya kati na matawi yake yote
ambayo ni kutoka Dar salaam kwenda kigoma, Uvinza hadi Msongati kwa
ajili ya mizigo ya Burundi.
Alisema kuwa tawi jingine ni
lile la kutoka Tabora hadi Kalemi kwa ajili ya mizigo ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na ile ya kutoka Tabora kupitia Shinyanga
hadi Mwanza kwa ajili ya Ukanda wa ziwa.
Kwa upande wa Msemaji wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. James Mbati akiwalisha maoni ya Kambi
hiyo alisema kuwa reli ya kati ikiboreshwa itasaidia kutwala soko la
usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi kama vile DRC,
Burundi , Uganda na Rwanda.
Alisema kuwa hivi watanzania
wanatakiwa kuwa na reli ambayo itaendana na ya sasa inayowezesha
usafirishaji wa mizigo kwa kasi na uwezo mkubwa wa kubeba mzigo mzito.
Mhe. Mbati alishauri kuwa ili
kufupisha ujenzi wa reli hiyo ni vema kukawa na wakandarasi ambao
watapewa vipande vidogo vidogo vya takribani kilometa 200 ambavyo
vitajengwa kwa wakati.
Naye Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbalawa alisema kuwa Serikali kupitia
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli(RAHACO) inaendelea na uboreshaji wa
miundo mbinu ya reli ili kuongeza uwezo wa njia zilizopo za reli ya kati
za kubeba mizigo mizito zaidi.
Alisema kuwa mara ya
kukakamilisha kwa uboreshaji wa reli hiyo kutasaidia uhimilivu wa
mwendo kasi wa juu na kupunguza ajli za treni.
Wizara hiyo imeliomba Bunge
kuidhinisha shilingi 4,895,279,317,500.00 kwa ajili ya utekelezaji wa
majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha ujao.
Kati ya fedha hizo shilingi
2,212,141,496,500.00 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, shilingi
2,587,333,762,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi na shilingi 95,
804,059,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya mawasiliano.
No comments:
Post a Comment