Na Masanja Mabula –Pemba
WANANCHI wa Kisiwani Pemba wamesema kwamba wamechoshwa na vitendo nenda rudi nenda rudi katika Ofisi za vizazi na vifo kufuatailia vyeti vya kuzaliwa na pamoja na vyeti vya vifo ambavyo upatikanaji wake unasumbua.
Wananchi hao wamelalamika juu ya ucheleweshwaji wa vyeti hivyo jambo ambalo limekuwa nikikwazo kikubwa katika upatikanaji wa haki zao za msingi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wamesema kuwa upatikanaji wa vyeti hivyo ni tatizo la muda mrefu hali ambayo imesababisha baadhi wa watoto kuanza skuli bila ya kuwa na cheti cha kuzaliwa .
Aisha Kombo Hassan Mkaazi wa Ukutini Mkoani alisema kwamba ufuatiliaji wa vyeti katika ofisi za Vizazi na Vifo za Wilaya, mbali na usumbufu anaoupata pia umekuwa ukiongeza gharama anazotumia katika gari za abiria.
"Hata ukikipata cheti utakuwa imetumia zaidi ya shilingi elfu ishirini, hii ni kutokana na gharama za kupanda katika gari za abiria mara kwa mara kwa kweli tunasumbuka sana," alifahamisha.
Naye Juma Ali Mohammed mkaazi wa Makangale, alisema kwamba wapo baadhi ya wananchi wamekosa vitambulisho vya mzanzibar mkaazi kutokana na kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Alisema wako vijana ambao wametmiza umri wa kupiga kura , lakini wameshindwa kupata fursa hiyo kutokana na kutkuwa na vyeti vya kuzaliwa ambavyo ndiyo vinavyopelekea kupata kitambulisho cha Mzanzibar .
Hali hiyo pia imelalamikiwa na Mwatime Omar Issa Jojo Mchangamdogo , ambaye aliiomba Serikali kuchukua hatua za makusudi kulipatia ufumbuzi suala hilo, ili wananchi wanaondokane na usumbufu wanaoupata kwa sasa.
Kwa upande wake Mdhamini Ofisi ya Wakala Wa Usajili Wa Biashara Na Mali Vizazi Na Vifo Pemba Salehe Mohd Abdalla amesema hali hiyo inatokana na ufinyu wa bajeti katika Ofisi hiyo .
Alisema kuwa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni kwani Ofisi hiyo inatagemea kupata magamba elfu kumi (10000) kutoka Ofisi Kuu Unguja na watayagawanya kwa Ofisi za Wilaya zote Pemba.
"Tunatarajia kupata magamba elfu kumi , na yakifika tu tunayapeleka katika Ofisi za Vizazi za Wilaya , naomba sana wananchi wawe wastahamilivu tatizo linafahamika," alieleza.
Aidha alifahamisha kuwa kutokana na ongezeko la vizazi, ofisi ya Pemba inahitaji kupata magamba angalau mia tatu (300) kila mwezi ili kukidhi haja na mahitaji ya wananchi.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kwamba baadhi ya Wilaya kuna wananchi wanadai vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao kwa zaidi ya miaka mitano sasa bila ya mafanikio.
No comments:
Post a Comment