Pages

Thursday, August 29, 2013

WAZIRI LUKUVI NA WABUNGE 'WAUZA UNGA'


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wiliam Lukuvi amesema kwamba wabunge wengi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuonya kwamba iwapo Serikali italazimika kuwataja hakuna mbunge yeyote atakayesalimika.
 
Waziri Lukuvi ambaye anashughulikia masuala ya Bunge alitoa kauli hiyo bungeni juzi wakati akijibu maswali ya nyongeza ambapo wabunge waliitaka Serikali kutaja majina ya vigogo wanaojihusisha na biashara hiyo.
 
Mmoja wa wabunge hao alimuuliza kama Serikali inaweza kuwaeleza Watanzania kuhusu ukubwa wa biashara hiyo nchini, wakati mbunge mwingine alihoji sababu za Serikali kushikwa kigugumizi kila inapotakiwa kutaja majina ya magwiji wauza ‘unga’.
 
Zipo tetesi kuwa, kauli ya waziri huyo kwamba wabunge wengi wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo inaweza kuwa imetolewa kama mbinu ya kuwanyamazisha wabunge ili waingiwe hofu na kujenga dhana kwamba hakuna mbunge miongoni mwao aliye msafi.
 
Hatudhani kama ungekuwapo utata iwapo waziri huyo angesema baadhi ya wabunge wanadaiwa kufanya biashara hiyo, kwani wananchi wengi wamekuwa wakijua jambo hilo kwa muda mrefu. Siyo siri kuwa, kwa muda mrefu baadhi ya wabunge walikuwa wakitajwa kujihusisha na biashara hiyo hata kabla hawajaingia bungeni.
 
Hata hivyo, yafaa ieleweke kwamba jambo linalogomba hapa ni kauli kwamba wabunge wengi wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo. Ndio maana tunadhani kuwa, hakuna anayeweza kubisha kwamba kauli ya Waziri Lukuvi ni nzito mno na inaliweka Bunge njia panda kwa wabunge wake wengi kukabiliwa na tuhuma nzito kama hizo.
 
Ni kauli ambayo bila shaka imechafua taswira ya Bunge machoni mwa wananchi na imeibua maswali mengi kuhusu hadhi ya Bunge na wabunge wenyewe.
 
Pengine ndio maana baadhi ya wabunge walimtaka Waziri Lukuvi kufuta kauli yake hiyo kwa maelezo kwamba siyo tu ni ya jumla mno, bali pia kwamba imelichafua Bunge. Bila shaka wabunge hao walitaka kuonyesha kwamba wao ni wasafi, hivyo tunadhani hawakutendewa haki kwa kulundikwa katika kapu moja na wabunge waovu.
 
Tunadhani kauli ya Waziri Lukuvi kwamba iwapo Serikali italazimika kuwataja watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya hakuna mbunge atakayesalimika haikuwa ya busara na ilitolewa tu kwa kukurupuka baada ya wabunge kumzomea.
 
Vinginevyo, Waziri alipaswa kujua unyeti wa suala hilo hasa kwa kutilia maanani kwamba Rais Jakaya Kikwete miaka minne hivi iliyopita alisema ana orodha ya magwiji wa ‘unga’ , lakini hadi leo hajapata ujasiri wa kuyaweka bayana.
 
Kwa misingi hiyo, nani anaweza kuamini kwamba Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo kwa nia njema? Tunasema hivyo kwa sababu kauli hiyo ilijenga dhana potofu kwamba wabunge wote, wakiwamo Spika, Waziri Mkuu na mawaziri wanajihusisha na biashara hiyo haramu.
 
Ni kauli ambayo tunaweza kusema inadhihirisha kwamba Serikali sio tu imekata tamaa katika vita dhidi ya biashara hiyo, bali pia kwamba sasa iko njia panda na haijui nini la kufanya.

Source:  Mwananchi.co.tz

No comments: