*************************
TUME ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwakumbusha wananchi kuwa mwisho wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa asasi, taasisi, na makundi ya watu yenye malengo yanayofanana ni siku ya Jumamosi, tarehe 31 Agosti 2013.
Tarehe 31 Agosti, 2013 ilipangwa na kutangazwa katika Mwongozo Kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu Wenye Malengo Yanayofanana uliotolewa na Tume na ulianza kutumika tarehe 01 Juni 2013.
UTARATIBU WA KUWASILISHA MAONI
Kwa mujibu wa Aya Na. 4.0 ya mwongozo huo, Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo yanayofanana yanatakiwa kuwasilisha kwa Tume maoni hayo kwa njia ya randama, barua, andiko au muhtasari wa makubaliano, n.k.
Hivyo basi Asasi, Taasisi au Makundi ya watu wenye Malengo yanayofanana yanaweza kupeleka maoni yao moja kwa moja katika ofisi za Tume zilizopo jijini Dar es Salaam, Mtaa wa Ohio au Zanzibar, Mtaa wa Kikwajuni, Gofu Jengo la Mfuko wa Barabara. Aidha, wanaweza kutuma maoni hayo kwa kutumia barua pepe ambayo ni katibu@katiba.go.tz au anuani zifuatazo:
1.Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 1681, Dar es Salaam; au
2.Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 2775, Zanzibar.
Muda wa Kuwasilisha Hautaongezwa
Tume inapenda kusisitiza kuwa muda wa kupokea maoni kuhusu Rasimu ya Katiba hautaongezwa na kuwa Asasi, Taasisi na Makundi ya watu wenye Malengo yanayofanana kuzingatia tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maoni iliyopangwa na Tume.
No comments:
Post a Comment