Pages

Monday, July 22, 2013

SERIKALI YAAHIDI KUSHUGHULIKIA MAPENDEKEZO YA TOZO YA KODI ZA SIMU

Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa akisisitiza jambo juu ya tozo ya kodi katika laini za simu wakati alipokutana na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Maelezo).


Na Eliphace Marwa (MAELEZO)

SERIKALI imewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kuhusiana na mpango wa ukusanyaji wa kodi ya laini za simu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Mgimwa amesema kuwa Serikali inaendelea kukutana na wadau mbalimbali ili kujadili na kupokea mapendekezo kuhusiana na dhamira ya serikali kutoza kodi kutoka katika laini za simu.

Aliongeza kuwa serikali ina nia njema ya kuongeza mapato yake ili kuongeza kasi ya kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake hususani wa vijijini.

"Lengo hasa la kodi hii ni kuboresha huduma za msingi vijijini kama umeme, maji na barabara ambazo ni duni sana vijijini, hata hivyo tunafanyia kazi mapendekexo mbalimbali ya wananchi na wadau wenye mitizamo mbalimbali" alisema Dkt. Mgimwa.

Aidha Dkt. Mgimwa mesema kuwa hivi karibuni amekutana na chombo cha watoa huduma za mawasiliano (MoAT) na kujadiliana nao na kuwaahidi kuwa mapendekezo yao yatafanyiwa kazi.

Mkutano huo umekuja baada ya wadau mbalimbali kutoa malalamiko juu ya uwepo wa tozo ya kodi ya laini za simu ambapo mmiliki wa laini ya simu atatakiwa kulipa gharama ya shilingi 1,000 kila mwezi mara kodi hiyo itakapoanza kutozwa.

No comments: