Pages

Tuesday, July 30, 2013

NIKO TAYARI KUPIGWA RISASI AU KUNYONGWA HADHARANI - Iddi Azzan




Na Ipyana Mwaipaja

Mheshimiwa Iddi Azzan, mbunge wa jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya CCM amesema kuwa yupo tayari kupigwa risasi au kunyongwa hadharani iwapo atagundulika kujihusisha kwa vyovyote na madawa ya kulevya.

Amesema maneno hayo leo asubuhi alipokuwa anahojiwa na kituo cha Radio One katika kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kupitia njia ya simu ambapo mbunge huyo amekana kuhusika kwa lolote na biashara hiyo haramu.

“Napenda kuwahakikishia watanzania kuwa sihusiki kwa aina yoyote na biashara ya madawa ya kulevya wala biashara yoyote haramu na iwapo nitagundulika kuhusika basi niko radhi kupigwa risasi au kunyongwa hadharani,” amesema Azzan.

Aidha mbunge huyo amesema kuwa anaamini hizo ni njama za kumchafua ambazo zinafanywa na wabaya wake ili kumharibia katika uchaguzi wa mwaka 2015 kwa sababu wanajua yeye ana nafasi kubwa ya kuwashinda.

“Najua ni mapambano ya 2015 yameanza kwaiyo wabaya wangu ndio wameanza kunichafua ili kuniharibia, lakini nataka niwahakikishie watanzania kuwa mimi ni mtu safi na nitaendelea kuwatumikia kwa uadilifu kama ilivyokuwa siku zote” amesema Azzan.

Hata hivyo mbunge huyo amekiri kuwa hii ni mara ya pili kwa yeye kuhusishwa na madawa ya kulevya na kwamba jana yeye mwenyewe ameripoti Polisi na kuwaambia kuwa wafanye uchunguzi na kama atabainika kujihusisha na biashara hiyo basi achukuliwe hatua za kisheria.

Mhe. Azzan pia ameliomba jeshi la polisi kuwachukulia hatua wanaomvumishia mambo hayo pindi itakapogundulika kuwa hahusiki na biashara hiyo, ili kukomesha tabia hiyo ambayo amesema inaelekea kukua kutokana na sababu za chuki na maslahi binafsi ya watu.

No comments: